Wanawake wa Salaf hawakuwa wakiyatembelea makaburi


Maoni sahihi ni kwamba ni haramu kwa mwanamke kukusudia kutoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kuyatembelea makaburi. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wanaoyatembelea makaburi, na katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Mtume  wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanawake wanaoyatembelea makaburi na wale wenye kuyafanya ni mahali pa kuswalia na wenye kuyatia mataa.”[1]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ameraddi ukosoaji wa Hadiyth hizi mbili katika “al-Majmuu´-ul-Fataawaa”. Miongoni mwa aliyosema ni kuwa jumla inayosema (زوارات) inaweza kuwa inakusudia ule wingi wa wanawake wanaoyatembelea na si kile kitendo cha mmoja wao kuyatembelea mara kwa mara. Ametilia nguvu hoja yake kwa maneno Yake (Ta´ala):

حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا

“… mpaka watakapoifikia na ikafunguliwa milango yake.”[2]

Kwa kukazia herufi (ت).

Lakini ikitokea mwanamke ameyapitia makaburi pasi na kukusudia na akawatolea salamu, basi kitendo hicho hakina neno – Allaah akitaka. Pengine akajengea hoja kwa Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) isemayo:

“Jibriyl alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika Mola wako anakwamrisha kuwaendea watu wa al-Baqiy´ uwaombee msamaha.” Nikasema: “Niwaambie nini, ee Mtume wa Allaah?” Sema:

السَّلامُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الدِّيَارِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُسْلِمِين,و يرحم الله المستقدمين منا و المستأخرين,وَإِنَّا إِنْ شَاءَ اللهُ بكم لاحِقُونَ نَسْأَلُ الله لَنَا وَلَكُمْ الْعَافِية

“Amani ishuke juu yenu, watu wa nyumba za waumini na waislamu. Allaah awarehemu wale waliotangulia katika sisi na wanaokuja nyuma. Na sisi – atakapo Allaah – tutakutana na nyinyi. Namuomba Allaah atupe sisi na nyinyi afya njema.”[3]

Udhahiri ni kwamba alimuuliza ni nini atachosema ikiwa atawatembelea. Hata hivyo si jambo la wazi kwamba kuna uwezekano akawaombea du´aa hii bila ya kuwatembelea. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kutokana na tunavojua hakuna yeyote katika maimamu ambaye amependekeza kwao kuyatembelea makaburi. Wanawake katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah waongofu hawakuwa wakiyatembelea makaburi kama yanavotembelewa na wanamme.”[4]

[1] Abu Daawuud (3236), at-Tirmidhiy (320), an-Nasaa’iy (2043) na Ahmad (2030). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (225).

[2] 39:73

[3] Muslim (974).

[4] Majmûu´-ul-Fataawaa (24/345).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/323-324)
  • Imechapishwa: 02/08/2021