Wanaosherehekea maulidi ni moja kati ya mawili


Mpaka hapa tumepata kujua kuwa, kusherehekea Maulidi ya Mtume ni Bid´ah bila ya shaka. Na ni wajibu kuiacha na wala haijuzu kuifanya. Na yule atakayeyafanya, yuko baina ya mambo mawili:

1) Ima ni mjinga hajui haki, afunzwe na kuongozwa.

2) Au ni mwenye kasumba za kufuata matamanio na kiburi. Alinganiwe katika usawa na aombewe uongofu na Tawfiyq. Na katika watu wote hawa wawili hakuna mwenye hoja, sawa huyu wa kwanza ambaye ni mjinga wala huyu wa pili mwenye kasumba. Wote hawana hoja. Hoja inapatikana katika Aliyosema Allaah na Mtume Wake. Na sio katika kauli isiyokuwa ya hao wawili. Kisha kusema kuwa Bid´ah imegawanyika sehemu mbili; Bid´ah nzuri na mbaya, na katika Haramu na wajibu, huku ni kutoa kauli pasina dalili. Na wameliradi hilo Ahl-ul-´Ilm wal-Yaqiyn na kubainisha makosa ya mgawanyo huu. Na wametumia dalili kwa kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayezusha katika Amri yetu hii yasiyokuwemo, basi yatarudishwa.” (Muttafaq)

Na Imaam Muslim kapokea katika Swahiyh yake, Hadiyth kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha)ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasema:

“Atakayefanya ´amali isiyokuwa humo na Amri yetu, basi itarudishwa.”

Na katika Swahiyh, Hadiyth kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikhutubu siku ya Ijumaa akisema: “Amma ba´ad: “Hakika maneno bora ni Kitabu cha Allaah, na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na shari ya mambo ni mambo ya kuzua na kila Bid´ah na upotofu.”

Na wala hakugawa na kusema: “Kuna Bid´ah hii na hii.” Bali kasema: “… kila Bid´ah ni upotevu”. Bali alizidi kusisitiza hilo kwa kusema: “Tahadharini na mambo ya kuzusha! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah, na kila Bid´ah ni upotevu.”

Na Bid´ah inakuwa katika mambo ya Dini ambayo ni ya kujikurubisha na si katika mambo ya dunia. Ama mambo ya dunia; katika mambo ya kula na kunywa, kukafanywa chakula maalumu na cha aina mbalimbali, hili halina neno. Bali kinachozungumziwa ni katika mambo ya kujikurubisha na mambo ya ´Ibaadah ambayo mtu anajikurubisha kwayo kwa Allaah, hapa ndio mahala pa kuzua. Hali kadhalika, uvumbuzi wa mambo na vifaa vya vita; wanaweza kuzua mambo mbalimbali katika silaha za kijihami na kujitetea, hili halina neno. Kinachozungumziwa ni katika mambo ambayo mtu anajikurubisha kwayo kwa Allaah, na ambayo yanachukuliwa kwa watu kuwa ni ukurubisho na ni utiifu kwa Allaah, wakitarajia kwa hayo thawabu kutoka kwa Allaah. Hapa ndipo panapozingatiwa. Yale ambayo hayakufanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah wake na wala hakulitolea dalili (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kuliashiria, bali limezua watu na na kulitia katika Dini ya Allaah, hilo ni Bid´ah. Sawa ikiwa fulani atapenda au atachukia. Na haki ndio yenye haki kufuatwa. Katika mlango huu kuna mengi yamezushwa na watu; kama ya kujenga Misikiti katika makaburi na kuyawekea kuba, hizi ni Bid´ah ambazo zimezua shari nyingi. Mpaka imejitokeza Shirki kubwa na kufikia makaburi kuabudiwa badala ya Allaah kwa sababu ya Bid´ah hii (ya Maulidi). Ni wajibu kwa Muislamu atanabahi na kushikamana na Aliyoyawekea Allaah Shari´ah, na atanabahi na waliyozusha watu na atahadhari nayo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Nuur ´alaad-Darb (770)
  • Imechapishwa: 12/03/2018