Muislamu anatakiwa kuwa mwenye kufuata na si mwenye kuzusha. Kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa kumfuata na si kwa mambo yaliyozuliwa ambayo hawakuyajua Maswahabah wala waliowafuata kwa wema.

Baadhi ya watu wanasema kuwa malengo yao ni mazuri na kwamba wanafanya kitu hichi kwa malengo mazuri na kwamba malengo yao mazuri ndio wanayotarajia Allaah kuwasamehe. Ni jambo linalojulikana kuwa malengo mazuri ni lazima yaafikiane na Sunnah. Haitoshi kwa mtu kufanya kitu kisichokuwa na msingi wowote katika dini kisha akasema kuwa eti malengo yake ni mazuri. Miongoni mwa mambo yanayoweka wazi jambo hilo ni kwamba kuna Swahabah mmoja  mtukufu (Radhiya Allaahu ´anh) alichinja Udhhiyah yake kabla ya swalah ya ´iyd siku ya kuchinja. Malengo yake yalikuwa mazuri; malengo yake ilikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wakija kutoka kuswali swalah ya ´iyd kichinjwa chake kiwe kimeshakuwa tayari na kiwe ndicho cha kwanza kuliwa katika vichinjwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipojua kuwa amechinja kabla ya kuswali akamwambia:

“Kondoo wako ni kondoo wa nyama.”

Bi maana sio Udhhiyah kwa sababu hakukichinja katika wakati wake. Wakati wa Udhhiyah ni baada ya swalah na si kabla ya swalah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akichinja Udhhiyah baada ya kumaliza kuswali. Huyu ambaye alichinja kabla ya swalah ya ´iyd malengo yake yalikuwa mazuri na mema. Lakini pamoja na hivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

“Kondoo wako ni kondoo wa nyama na sio Udhhiyah.”

Kondoo wa nyama maana yake ni kama mfano wa kondoo anayechinjwa katika mwezi wa Muharram, Swafar, Rabiy´, Rajab, Sha´baan, Ramadhaan na wakati mwingine wowote ambapo watu wanachinja kwa ajili ya kula nyama.

Kwa ajili hiyo Haafidhw Ibn Hajar katika “Fath-ul-Baariy” wakati alipokuwa akitoa maelezo ya Hadiyth hii amesema akinukuu kutoka kwa baadhi ya wanachuoni:

“Hapa kuna dalili juu ya kwamba kitendo ni lazima kiafikiane na Sunnah. Haitoshi lengo zuri la mtendaji ili kitendo hicho kiwe chenye kukubalika na kimsaidie mwenye nacho.”

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bid´at-ul-Mawaalid wa mahabbat-in-Nabiyy http://www.ajurry.com/vb/showthread.php?t=36078
  • Imechapishwa: 05/11/2019