Wakati maalum wa Laylat-ul-Qadr

Wanachuoni wametofautiana kama usiku wa Qadr umebaki au ulikuweko wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake. Maoni sahihi ni kwamba bado ni wenye kuendelea.

Je, unakuwa mwaka mzima au unakuwa katika Ramadhaan peke yake? Ni jambo wanachuoni wametofautiana. Jopo la wanachuoni wengi ni wenye kuonelea kuwa unakuwa katika Ramadhaan. Ibn Mas´uud anaonelea kuwa unakuwa mwaka mzima.

Jengine ni kwamba wale wenye kuoenelea kuwa unatokea katika Ramadhaan wametofautiana wakati wake maalum katika Ramadhaan. Jopo la wanachuoni wanaonelea kuwa unatokea katika zile siku kumi za mwisho. Hadiyth nyingi Swahiyh zinajulisha juu ya jambo hili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni katika zile siku kumi za mwisho katika Ramadhaan na utafuteni katika kila usiku wa witiri; tarehe tisa ni wenye kubaki, tarehe saba ni wenye kubaki na tarehe tano ni wenye kubaki.”[1]

Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni katika tarehe tisa ni wenye kubaki, tarehe saba ni wenye kubaki, tarehe tano ni wenye kubaki, tarehe tatu ni wenye kubaki na usiku wa mwisho.”[2]

Maoni ya pili yanasema kwamba unakuwa Ramadhaan nzima. Haya ni maoni ya al-Hasan al-Baswriy.

Wale wenye kuonelea kuwa unatokea katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan wametofautiana kama unatokea katika zile nyusiku za witiri peke yake au pia katika nyusiku za shufwa. Jopo la wanachuoni wengi wanaonelea kuwa unatokea katika nyusiku za witiri. Hadiyth zote Swahiyh zinajulisha hivo. Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni katika zile siku kumi za mwisho ambazo ni witiri.”[3]

Maoni ya pili yanasema kuwa unaweza kutokea katika nyusiku za shufwa kama unavotokea katika nyusiku za witiri. Haya yamesemwa na al-Hasan. Imesimuliwa kwamba al-Hasan na Maalik wote wawili wamesema:

“Usiku wa Qadr ni usiku wa tarehe kumi na nane.”

[1] al-Bukhaariy (2021) na Muslim (1165).

[2] at-Tirmidhiy (794) ambaye ameisahihisha, al-Haakim (1/438), Ahmad (5/36), Ibn Khuzaymah (2175), Abu Daawuud at-Twayaalisiy (881) na al-Bayhaqiy katika “Shu´b-ul-Iymaan (3681). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (794).

[3] al-Bukhaariy (2021) na Muslim (1165).

  • Mhusika: Haafidhw ´Abdur-Rahmaan bin al-Jawziy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad-ul-Masiyr (4/469-470)
  • Imechapishwa: 14/05/2020