Himdi zote njema anastahikii Allaah na swalah na salamu zimwendee Mtume wa Allaah, familia yake, Maswahabah zake na wale wenye kufuata uongofu wake.

Amma ba´d:

Miongoni mwa mambo ambayo Allaah Amewapa majaribio Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwayo, ni kupatikana idadi kubwa ya watu wa batili na wale wanaowasaidia pamoja na kuenea kwa Bid´ah na wale wanaowapa nguvu. Lakini hapana shaka yoyote kwamba ahadi ya Allaah (Subhaanahu) ni yenye kitimizwa. Ameahidi (Jalla wa ´Alaa) kuihifadhi Dini Yake pale Aliposema:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi Tumeteremsha Ukumbusho huu na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaouhifadhi.” (15:09)

Katika kuihifadhi Kwake Dini Yake na Ukumbusho Wake ni kusahilisha kwa wanaume wa kisawasawa katika Ummah huu kuilinda Dini Yake kutokamana na upotoshaji wa wenye kupetuka mpaka, dhana za wakanushaji na tafsiri mbovu za wajinga. Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliilinda Dini Yake, Kitabu Chake na Mtume Wake kwa ndimi zao na mikuki yao. Kamwe hawakuchoka kuhami usafi wa Dini hii. Kisha wakafuatwa kwa hilo na Taabi´uun wabora na halafu waliowafuata mpaka wakati wetu huu leo na mpaka pale Qiyaamah kitaposimama.

Miongoni mwa wanaume hawa imara ambao wameweka juhudi kubwa kabisa katika kuilinda Dini Yake, kuliweka juu Neno Lake na kuzisafisha fikira za watu kutokamana na ukhurafi wa makhurafi, upotevu wa wapotevu, Bid´ah za watu wa Bid´ah na yasiyokuwa hayo katika aina mbalimbali za upotevu, si mwengine ni Shaykh, ´Allaamah na mpambanaji Jihaad Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy (Hafidhwahu Allaah). Anatumia juhudi kubwa awezazo kuupa nasaha Ummah huu. Ametumia wakati wake na umri wake kuwaelekeza vijana wa Waislamu na amekifungua kifua chake na nyumba yake kwa kila anayetaka haki na kujitahidi kuiendea.

Lakini Sunnah ya Allaah kwa waja Wake ni kwamba Anawapa majaribio na mitihani na wala hutopata mabadiliko katika desturi ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

ألم، أَحَسِبَ النَّاسُ أَنْ يُتْرَكُوا أَنْ يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لا يُفْتَنُونَ

“Alif Laam Miym. Je, wanadhani watu kwamba wataachwa wanasema: “Tumeamini.” basi ndio wasijaribiwe?” (29:02)

Miongoni mwa majaribio hayo ambayo amepewa Imaam huyu ni msimamo wa Ahl-ul-Bid´ah dhidi yake na majaribio yao mabaya kwa njia zote zinazowezekana kumpiga vita na kumwangusha, kwa kuwa wao waonavyo ni kwamba lengo zuri linaitakasa njia. Wametumia uongo, uzushi, dhuluma, batili, ghushi, matusi na tabia na sifa zingine zote za shari na za ki-Shaytwaan.

Lakini (Hafidhwahu Allaah) amekuwa ni ngangari kama mlima ulio imara. Njia zote hizi hazikumfanya kutoka nje katika mwenendo waliokuwemo waliotangulia. Wala hazikumfanya akaacha kuenenza Dini ya Allaah na Mtume Wake, kusafisha kwake Bid´ah zote, unafiki, maasi na madhambi na kuwafichukua wale ambao wamejivisha kivazi cha Sunnah na wakati wako mbali na Sunnah. Yote haya ni katika fadhilah na neema za Allaah juu yake zisizohesabika.

Usiku na mchana, Ahl-ul-Bid´ah, waongo na wasaidizi wao, kwa siri na kwa dhahiri, wanajitahidi kumwangusha chini ili mfumo wa kinabii anaoueneza kwa watu uweze kuanguka na badala yake bendera ya Bid´ah na upotevu iweze kushika nafasi.

Wameandika “ar-Radd al-Wajiyz” dhidi yake na akaijibu kwa “an-Naswr al- ´Aziyz”. Waliandika uongo wao, akawafichukua na wakaanguka chini. Namna hii Allaah Anainusuru Dini Yake na waja Wake waumini.

Aina hii ya mnyororo ni mrefu na ni yenye kuendelea kila siku, lakini unaanguka mara moja mbele ya haki – na himdi zote ni za Allah. Hilo ni kwa sababu mlango wa uongo ni mpana na milango ya upotevu iko wazi, wakati adhabu ya uongo ni kuufichua na kuufedhehesha na mwisho mwema ni wa wenye kumcha Allaah.

Matusi na maapizo yote haya yanayotoka kwa watu wa matamanio na wajinga ni madhambi kwao na wakati huohuo Shaykh Rabiy´ analipwa thawabu kwayo. Kadhalika hali ni hivo kwa Maswahabah, Taabi´uun na waliokuja baada yao. Raafidhwah, Khawaarij, Mu´tazilah au Ahl-ul-Bid´ah wengine wote hawajapatapo kuwatukana isipokuwa inakuwa ni matendo mema katika mizani ya wema wetu waliotangulia na Allaah Ananyanyua manzilah zao, hata kama hilo litakuwa baada ya kufa kwao. Kwenye macho ya Ahl-ul-Haqq was-Sunnah hilo haliwadhuru kitu. Ni mara ngapi Raafidhwah wamemtukana Abu Bakr na ´Umar? Ni mara ngapi ´Ashaa´irah, Mu´tazilah na Jahmiyyah wamemtukana Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah? Ni mara ngapi maadui wa Tawhiyd, wenye kuinusuru shirki na Ahl-ul-Bid´ah wamemtukana Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab? Ni mara ngapi maadui wa Sunnah wamewatukana wanachuoni na maimamu wetu kama Shaykh Ibn Baaz, Shaykh al-Albaaniy, Shaykh Ibn ´Uthaymiyn, Shaykh al-Fawzaan, Shaykh Rabiy´ na wengineo? Wao ni kama jinsi Shaykh ´Abdul-Latwiyf bin ´Abdir-Rahmaan bin Hasan Aal ash-Shaykh (Rahimahu Allaah) alivyosema wakati alipokuwa anazungumzia kuhusu babu yake, Mujaddid na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab:

“Ana fadhilah na athari, jambo ambalo halifichikani kwa watu waheshimiwa na wenye ufahamu. Miongoni mwa mambo maalum ambayo Allaah Amemtofautisha nayo katika karama, ni kwamba aliwashinda maadui wa Dini na wapinzani wa waja wa Allaah waumini, wakati huo ndipo wakamtukana, kumsemea uongo na kutaja mapungufu yake.”[1]

Hali kadhalika kunapatikana kundi ambalo linamtukana Shaykh Rabiy´, kumtuhumu uongo na kumbeza, kunapatikana kundi vilevile linalomsifu kwa sifa za mdomo zinazozingatiwa na kumpendekeza kwa mapendekezo yanayokubalika. Wanachuoni wote wa Sunnah na wanafunzi wenye inswaaf waliosalimika na mambo ya ushabiki na matamanio wanajua fadhilah za mtu huyu – lakini fadhilah hazijui yeyote isipokuwa zinajulikana na watu wa fadhilah.

Amesifiwa na wanachuoni wa zama hizi. Wameshuhudia juu yake kwa ushuhuda wa haki na wa kweli na wamezungumzia kuhusu fadhilah zake, elimu yake na uthabiti wake juu ya Sunnah na juu ya mfumo wa wema waliotangulia (Salaf-us-Swaalih). Miongoni mwa wanachuon hawa watukufu ni Imaam Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz; Shaykh, ´Allaamah na Muhaddith Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy; Shaykh na ´Allaamah Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn; Shaykh Swaalih bin al-Fawzaan; Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab al-Bannaa; Shaykh Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy; Shaykh Muhammad bin ´Abdillaah as-Subayyil; Shaykh Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy; Shaykh Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy; Shaykh Swaalih as-Suhaymiy; Shaykh ´Ubayd al-Jaabiriy na wengineo katika wanachuoni, waheshimiwa na watu wema na wenye kheri. Hawa ndio wanachuoni na ushahidi wa wanachuoni unatosheleza kuwa ni ushahidi. Na vipi usitoshelezi ilihali Allaah (Ta´ala) Amewatumia wanachuoni kama ushahidi katika Kitabu Chake Kitukufu juu ya Umoja Wake (Subhaanah). Amesema:

شَهِدَ اللَّهُ أَنَّهُ لا إِلَهَ إِلا هُوَ وَالْمَلائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِماً بِالْقِسْطِ لا إِلَهَ إِلا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

“Allaah Ameshuhudia kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye na Malaika, na wenye elimu [wote wameshuhudia kwamba Yeye] ni Mwenye kusimamisha [uumbaji Wake] kwa uadilifu – hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; Mwenye nguvu zisizoshindikana, Mwenye hekima.” (03:18)

Tumetaja baadhi ya matapo na sifa zao juu ya Imaam huyu mtukufu ili iweze kuwabainikia watu wote wenye busara ni manzilah ipi alionayo Shaykh huyu mtukufu na ili uongo na upotevu wa wale wanaomponda na kumsema vibaya uweze kufichuka.

Hebu twende katika maneno hayo – na kwa Allaah peke Yake tunaomba msaada.

[1] al-Hadiyyah as-Sunniyyah, uk. 131

  • Mhusika: Shaykh Khaalid bin Dhwahwiy adh-Dhwafayriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.rabee.net/ar/sharticles.php?cat=12&id=57
  • Imechapishwa: 27/11/2019