Usiku wa Qadr unaweza kuonekana?

Swali: Je, mtu kama mtu anaweza kuona usiku wa Qadr kwa macho yake? Wako wanaosema kuwa mtu akiweza kuona usiku wa Qadr basi anaona nuru mbinguni na mfano wa hayo. Ni vipi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliuona? Ni vipi mtu atajua kuwa ameuona usiku wa Qadr? Je, mtu anapata thawabu zake ingawa umejitokeza katika usiku huo ambao hakuweza kuuona?

Jibu: Usiku wa Qadr unaweza kuonekana kwa yule ambaye Allaah (Subhaanah) amemuwafikisha kuona alama zake. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakijulishwa nao kwa alama zake. Lakini kutoiona hakuzuii kupata fadhilah zake kwa yule atakayesimama kuswali kwa imani na kwa matarajio.

Muislamu anatakiwa kujipinda kuitafuta katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan. Hivyo ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivowaamrisha Maswahabah zake kufanya kwa kutafuta ujira na thawabu. Endapo kusimama kwake – ambako amesimama kuswali kwa imani na kwa matarajio – kutakutana na usiku huu basi anapata thawabu zake ingawa hakujua ni usiku gani. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayesimama kuswali Laylat-ul-Qadr kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yule atakayesimama kuswali hali ya kuutafuta kisha akawafikishwa nao, basi atasamehewa dhambi zake zilizotangulia na zinazokuja huko mbele.”[2]

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayojulisha kwamba miongoni mwa alama zake ni kuchomoza kwa jua asubuhi yake likiwa halina miale ya kuchoma. Ubayy bin Ka´b akiapa kuwa ni usiku wa tarehe ishirini na saba ambapo akijengea hoja kwa alama hii.

Maoni yenye nguvu ni kwamba ni usiku wenye kuhamahama katika nyusiku kumi zote hizi na zile nyusiku za witiri ni zenye matarajio makubwa zaidi. Hata hivyo usiku wa tarehe shirini na saba ni wenye nguvu zaidi.

Yule ambaye akajipinda kuswali, kusoma, kuomba du´aa na mema mengine katika nyusiku zote basi pasina shaka atakuwa ni mwenye kuupa usiku wa Qadr na pia atakuwa ni mwenye kufuzu kwa yale Allaah aliyomwahidi yule ambaye atausimama muda wa kuwa amefany hivo kwa imani.

[1] al-Bukhaariy (1901) na Muslim (7060).

[2] Ahmad (22205).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/432)
  • Imechapishwa: 14/05/2020