Usiku wa Qadr unakuwa katika zile nyusiku kumi za mwisho Ramadhaan

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf lile kumi la katikati la Ramadhaan. Mwaka mmoja akafanya I´tikaaf mpaka ilipofika usiku wa tarehe ishirini na moja, asubuhi ambayo kikawaida ndio anatoka kwenye I´tikaaf yake, akasema: “Yule mwenye kutaka kufanya I´tikaaf basi afanye I´tikaaf katika zile siku kumi za mwisho. Nimeota juu ya usiku huo kisha nikausahau. Nimejiona asubuhi nikisujudu ndani ya maji na udongo. Utafuteni katika zile siku kumi za mwisho na utafuteni katika zile nyusiku za witiri.” Usiku huo kukanyesha. Msikiti ulikuwa kama paa na maji yakanyesha juu yake. Nikaona namna ambavo paji la uso la Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lilikuwa na athari ya maji na udongo baada ya asubuhi ya tarehe ishirini na moja.”

Hadiyth hii inajulisha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf zile siku kumi za katikati za Ramadhaan ili kutafuta usiku wa Qadr. Muundo huu unaonyesha kwamba alifanya hivo mara nyingi.

al-Bukhaariy na Muslim wako upokezi mwingine unaosema kwamba alifanya I´tikaaf zile siku kumi za mwanzo halafu ndio akafanya I´tikaaf katika zile siku kumi za katikati. Kisha akasema:

“Nimejiwa na kuambiwa kwamba ni katika zile siku kumi za mwisho. Yule miongoni mwenu anayetaka kufanya I´tikaaf basi afanye hivo.”

Haya yanajulisha kwamba yalifanyika kabla ya kubainikiwa kwamba ni katika zile siku kumi za mwisho. Baada ya kubainikiwa alikuwa akifanya I´tikaaf katika zile siku kumi za mwisho mpaka alipoondoka duniani.”

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Latwaa’if-ul-Ma´aarif, uk. 242
  • Imechapishwa: 16/05/2020