Uongozi na ukhalifa unathibiti kwa mambo gani. Ukhalifah unathibiti kwa moja katika njia tatu:

1- Ahl-ul-Hall wal-´Aqd kuteua na kuchagua. Kwa msemo mwingine Ahl-ul-Hall wal-´Aqd wachague kiongozi. Uongozi wake unathibiti kwa kuchagua na kuteua kwao. Makusudio sio watu wote kuchagua kama inavyokuwa katika kupiga kura kwa leo ambapo kunakuwa mtu yeyote; wanawake, watoto, wenye busara na wendawazimu wote hawa wanapata kupiga kura. Hapana! Haya hayana lolote kuhusiana na Shari´ah.

Mfano wa hili ni jinsi uongozi wa Abu Bakr ulivyothibiti. Uongozi wake ulithibiti kwa Ahl-ul-Hall wal-´Aqd kumteua na kumchagua.

Uongozi pia wa ´Uthmaan ulithibiti namna hii wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipowaachia mashauriano kwa watu sita. Ndipo ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf akawa anashauriana na watu miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar tu na akahangaika kwa siku tatu mpaka hatimaye akaona kuwa watu wote wamependekeza ´Uthmaan. Baada ya hapo wakampa bay´ah na akapewa bay´ah na wale sita pia kukiwemo Muhaajiruun na Answaar. Uongozi wake ukawa umethibiti kwa Ahl-ul-Hall wal-´Aqd kumchagua na kumteua.

Vilevile uongozi wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambao ulithibiti kwa kuchaguliwa na kuteuliwa na wengi katika Ahl-ul-Hall wal-´Aqd. Alipewa bay´ah na wengi katika Ahl-ul-Hall wal-´Aqd tukitoa Mu´aawiyah na watu wa Shaam.

2- Uongozi unathibiti kwa kiongozi aliyetangulia kuacha anamteua mtu atayeshika nafasi yake baada yake.

Mfano wa hili ni kuthibiti kwa uongozi wa ´Umar bin al-Khattwaab. Hakika uongozi wake ulithibiti kwa Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) kuacha anamteua. Huu ni mfano wa kuthibiti kwa uongozi kwa kiongozi kuacha anausia.

3- Uongozi unathibiti kwa nguvu na kushinda. Mtu akiwashinda watu kwa silaha na ufalme wake na akashika nafasi, basi itakuwa ni wajibu kumsikiliza na kumtii na anakuwa ni kiongozi. Katika hali hii itakuwa ni wajibu kumsikiliza na kumtii. Dalili ya hili ni yale yaliyokuja katika Hadiyth ya Abu Dharr ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kipenzi changu ameniusia kusikiliza na kutii hata kama [kiongozi] atakuwa ni mja kiwete.” Muslim (648).

Akishinda kwa silaha zake hata kama atakuwa ni mja kiwete; bi maana amekatwa mikono, miguu, masikio na mdomo, ni wajibu kumsikiliza na kumtii. Lakini lau itakuwa kwa kuteua na kuchagua, tusingelimchagua. Akija mtu wa pili na kutaka kumpindua huyu wa kwanza, anauawa huyo wa pili. Mtu huyu wa pili amekuja kutaka kuwafarisha waislamu baada ya kukusanyika kwa yule wa kwanza. Kama ilivokuja katika Hadiyth ya Abu Sa´iyd katika “as-Swahiyh” ya Muslim kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wakipewa bay´ah viongozi wawili muueni yule wa pili katika wao.” Muslim (1853).

Kujengea juu ya hili viongozi wote wa Banu Umayyah, Banul-´Abbaas, waliokuja baada yao mpaka leo uongozi wao wote hawa umethibiti kwa kushinda na kutumia mabavu. Hakuna uongozi uliyothibiti kwa kuteua na kuchagua isipokuwa uongozi wa Makhaliyfah waongofu peke yao. Huu ndio ufafanuzi juu ya masuala haya. Ni wajibu kwa mwanafunzi ayatambue haya kutokana na umuhimu wake.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/762-764)
  • Imechapishwa: 18/05/2020