Uhakika wa madhehebu ya Ashaa´irah juu ya maneno ya Allaah

Hebu tuhame twende katika utata wa Ashaa´irah na dalili walizotumia kuthibitisha madhehebu yao juu ya Maneno ya Allaah. Ashaa´irah ni pote kubwa na wanajiita kuwa ni Ahl-us-Sunnah na Ta´wiyl zao zinapatikana katika vitabu ambavyo vipo na vimeenea mbele yenu, sawa katika vitabu vya Fiqh, Usuwl-ul-Fiqh, Tafsiyr ya Qur-aan ambavyo wanawagawia watu na vinginevyo. Vitabu hivi vinasomwa katika mashirika mengi ya kielimu na kwenginepo. Wanajiita kuwa ni Ahl-us-Sunnah katika zama nyingi. Ni lazima kwa mwanafunzi atambue uhakika wa madhehebu ya Ashaa´irah na kubainisha baadhi ya utata ambao wameung´ang´ania.

Uhakika wa madhehebu ya Ashaa´irah kuhusiana na Maneno ya Allaah wanasema kuwa ni maana iliosimama katika nafsi na ni Maneno yasiyokuwa na herufi wala sauti. Hakusikiki kitu kutoka katika Maneno ya Allaah (Ta´ala). Maneno Yake ni maana iliosimama katika nafsi na hayasikiki. Kuhusiana na yaliyopo katika misahafu ni ibara ya Maneno ya Allaah ambayo yameeleza Jibriyl na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yaliyomo katika msahafu wanasema kuwa ni Maneno ya Allaah kimajazi. Ukiwaambia baadhi ya Ashaa´irah ya kwamba kilichomo ndani ya msahafu ni Maneno ya Allaah wanasema kuwa ni kweli ni Maneno ya Allaah kwa ajili ya kutaka kupakana mafuta, lakini wakati wa majadiliano na kuweka wazi uhakika wa madhehebu yao wanasema kuwa ndani ya msahafu hakuna Maneno ya Allaah na sisi pale tunaposema kuwa ni Maneno ya Allaah tunamaanisha kuwa ni Maneno ya Allaah kimajazi kwa kuwa yanapelekea katika Maneno ya Allaah na ni dalili inayoonesha Maneno ya Allaah. Uhakika wa mambo Maneno ya Allaah yamesimama katika nafsi. Kwa ajili hii baadhi yao wanaweza kuukanyaga msahafu na miguu yao na kusema kuwa ndani yake hakuna Maneno ya Allaah – tunaomba kinga kwa Allaah.

Kuhusiana na ule mpangilio wenye kusikika katika misahafu ni dalili yenye kuonesha kuwa Qur-aan imeumbwa. Kujengea juu ya hili Qur-aan inakuwa ni yenye kugawanyika sehemu mbili au Maneno ya Allaah yanakuwa na sehemu mbili:

a) Nusu ya kwanza ni ile ambayo haikuumbwa. Nayo ni ile maana iliosimama katika nafsi kwa Mola.

b) Nusu ya pili ni ile ambayo imeumbwa. Nayo ni herufi zile zile na maneno anayosoma msomaji.

Vipi Jibriyl alijua yaliyomo ndani ya Nafsi ya Allaah? Wana maoni mbali mbali juu ya hili. Baadhi yao wanasema kuwa Allaah alimlazimisha Jibriyl akawa amefahamu Maneno yaliyosimama katika nafsi. Alitenzwa nguvu na hivyo akawa ameyaeleza. Hivyo Qur-aan ni ibara iliyoelezea Jibriyl. Ni kwa mfano uko na bubu asiyezungumza na akakuashiria kwa ishara halafu ukafahamu aliyokuashiria kisha ukayaandika. Watu hawa – tunaomba kinga kwa Allaah – wamemfanya Allaah ni kama bubu.

Wengine wakasema kuwa Jibriyl aliichukua kwenye Ubao Uliohifadhiwa.

Kwa hivyo uhakika wa madhehebu ya Ashaa´irah yanaafikiana na nusu ya madhehebu ya Mu´tazilah. Mu´tazilah wanasema kuwa Qur-aan imeumbwa sawa matamshi na maana yake. Ashaa´irah wanasema kuwa maana yake haikuumbwa na matamshi yake yameumbwa.

Kama jinsi vilevile Ashaa´irah wanashabihiana na manaswara kuhusiana na masuala ya kuamini kwao ´Iysaa. Manaswara wanaamini kuwa Iysaa yuko na sehemu mbili; yuko na sehemu ya uungu na sehemu ya uanaadamu.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/192-194)
  • Imechapishwa: 30/05/2020