Tafsiri ya Hadiyth “Msiyafanye majumba yenu kuwa makaburi”

Swali: Ni yapi makusudio ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiyafanye majumba yenu kuwa makaburi?”

Jibu: Wametofautiana ya maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msiyafanye majumba yenu kuwa makaburi” katika maoni mawili:

Ya kwanza: Kuna waliosema kuwa maana yake ni kwamba msiwazike maiti wenu ndani yake. Huu ndio udhahiri wa matamshi. Lakini kumethibiti kuhusu hayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuzikwa nyumbani kwake. Kumejibiwa ya kwamba ni katika mambo maalum kwake.

Ya pili: Kuna wengine wamesema kuwa maana yake ni kwamba msiyafanye majumba kama makaburi mkawa hamswali ndani yake. Kwa kuwa ni jambo wamekubaliana wote ya kwamba makaburini sio mahali pa kuswalia. Hili linatiliwa nguvu na yale yaliyokuja katika baadhi ya njia:

“Swalini baadhi ya swalah zenu majumbani na wala msiyafanye kuwa makaburi.”

Maana zote mbili ni sahihi. Kuzika majumbani ni njia inayopelekea katika shirki. Jengine ni kwamba desuturi ilizoeleka tangu wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka hii leo ni kuzikwa pamoja na waislamu. Sababu nyingine vilevile ni kwamba ni kitu kinachowatia dhiki wale warithi na huenda wakamuogopa. Isitoshe kunaweza kutokea matendo ya haramu yanayopingana na malengo ambayo ni kukumbuka Aakhirah.

Hadiyth hii inathibitisha ya kwamba makaburini sio sehemu ya kuswalia. Kuyafanya makaburi kuwa ni sehemu ya kuswalia ni sababu inayopelekea katika shirki.

Hadiyth hii inathibitisha vilevile ya kwamba bora ni mtu kuziswali baadhi ya swalah zake nyumbani. Nazo ni zile swalah za sunnah zote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah bora ya mtu ni nyumbani kwake isipokuwa zile za faradhi.”

Isipokuwa zile zilizothibiti katika Shari´ah ya kwamba zinatakiwa kuswaliwa msikitini. Mfano wa hizo ni swalah ya kupatwa kwa mwezi na kisimamo cha usiku Ramadhaan. Hili linahusu misikiti yote kukiwemo Makkah na al-Madiynah. Kuswali swalah ya sunnah nyumbani kwako ndio bora zaidi kutokana na kuenea kwa Hadiyth. Jengine ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema hivo ilihali yuko al-Madiynah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (02/235-236)
  • Imechapishwa: 04/06/2017