Swaalih Aalush-Shaykh Kuhusu Allaah Alimuumba Aadam Kwa Sura Yake

Swali: Ni ipi maana ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah alimuumba Aadam kwa sura Yake”?

Jibu: Kuizungumzia Hadiyth hii maneno yatarefuka. Lakini kwa kifupi ni kwamba sura iliyokusudiwa hapa ina maana ya sifa. Sura katika lugha husemwa kukikusudiwa sifa. Kumethibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariu na ya Muslim ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kundi la kwanza litaingia Peponi likiwa na sura ya mwezi.”

Bi maana likiwa na sifa ya mwezi katika kule kumeremeta kwake na kuangaza kwake. Kwa hivyo maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah alimuumba Aadam kwa sura Yake.”

Ina maana:

“Allaah alimuumba Aadam kwa sura ya ar-Rahmaan.”

Bi maana akiwa na sifa za ar-Rahmaan (Jalla Jallaaluh). Allaah akamtofautisha Aadam na viumbe wengine kwa kumfanya kuwa na sifa nyingi ikiwa ni pamoja na baadhi ya sifa alizonazo Allaah pia. Namaanisha akiwa na ule msingi wa sifa pamoja na wakati huo huo kuzingatia ya kwamba sifa za viumbe hazifanani na sifa za Muumba. Allaah ana usikizi na akamfanya Aadam vilevile kuwa na sifa ya usikizi. Allaah anasifika kuwa na sifa ya uso na akamfanya Aadam vilevile kuwa na sifa ya uso. Allaah anasifika kuwa na sifa ya mikono miwili na akamfanya Aadam pia kuwa na sifa ya mikono miwili. Anasifika (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwa na nguvu, uwezo, kuzungumza, hekima, kughadhibika, kuridhia, kucheka na sifa nyenginezo zilizothibiti. Yote haya ni kwa ajili ya kumuheshimisha Aadam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama tulivyowatajieni. Maana yake ni hii kwa kifupi.

Kwa hivyo hakuna cha ajabu katika Hadiyth hii. Hivyo ndivyo alivyosema ´Allaamah Ibn Qutaybah (Rahimahu Allaah) ya kwamba watu hawakuielewa na hatimaye wakaikataa. Allaah akamtofautisha Aadam na viumbe wengine.

Wanyama wanaweza kuwa na usikizi na uoni. Lakini wasiwe na kuyadiriki mambo, wasiwe na hekima, wasiwe na kuzungumza kwa njia maalum na mengineyo. Lakini yeye Aadam ametofautishwa na viumbe wengine kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) kumfanya kuwa na sifa anazoshirikiana Naye katika ule msingi wa sifa yenyewe. Hata hivyo hashirikiani na Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika ule ukamilifu wa maana yake na ile namna yake. Vinginevyo kuna mengi ya kuizungumzia. Watu wengi hawakuelewa makusudio yake wala uhakika wa maoni ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya hilo.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.ajurry.com/vb/showthread.php?t=34142
  • Imechapishwa: 28/01/2017