Sifa mbalimbali za kuswali Witr na wakati maamuma wanapotakiwa kunuia Witr

Swali: Wakati imamu anapoleta Takbiyr kwa ajili ya swalah ya Witr waswaliji wanakuwa hawajui kama Witr ni Rakaa´ tatu au nne. Maamuma wanatakiwa kufanya nini?

Jibu: Kwanza ndugu zetu wanatakiwa kujua kuwa zile Rakaa´ mbili ambazo watu wanaziita kuwa ni Shafa´ ni Witr. Pale tu ambapo imamu anapomaliza kuswali Tarawiyh na akasimama basi wewe unatakiwa kunuia Witr ijapokuwa atakuwa ni mwenye kuswali kuanzia zile Rakaa´ mbili za mwanzo. Kwa sababu kuswali Witr kwa Rakaa´ tatu kuna sifa mbili:

Sifa ya kwanza: Mtu anaweza kuswali Rakaa´ zote tatu kwa Tasliym moja na Tashahhud moja.

Sifa ya pili: Mtu anaweza pia kuswali Rakaa´ tatu kwa Tasliy mbili na Tashahhud mbili kwa njia ya kwamba akatoa Tasliym baada ya Rakaa´ mbili kisha akamalizia kwa ile Rakaa´ ya tatu.

Hizi ndio sifa ya kuwitiri kwa Rakaa´ tatu.

Mtu akiwitiri kwa Rakaa´ tano, anatakiwa kuziswali zote tano kwa Tashahhud moja na Tasliym moja.

Mtu akiwitiri kwa Rakaa´ saba, anatakiwa kuziswali zote tano kwa Tashahhud moja na Tasliym moja.

Mtu akiwitiri kwa Rakaa´ tisa, anatakiwa kuswali Rakaa´ nane kisha aende Tashahhud na asitoe salamu. Halafu asimame kwa ajili ya Rakaa´ ya tisa kisha ndio aende Tashahhud na atoe salamu. Kwa hiyo Witr ya Rakaa´ tisa inakuwa na Tashahhudd mbili na Tasliym moja.

Hivi ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Lakini sisi ambao ni maimamu twatakiwa kuwaswalisha maamuma namna hii; kuwaswalisha Witr Rakaa´ tano, saba na tisa? Hapana. Haya yanawatia watu uzito na yanawaudhi baadhi ya watu pale wanapohitajia kwenda haja kubwa na ndogo. Jengine ni kwamba baadhi ya watu wanaingiwa na mashaka na kuanza kujiuliza kama imamu hivi sasa anaswali Witr au Tarawiyh. Kwa kuwa hawajui.

Kuna baadhi ya maimamu wanafanya hivo kwa kudai kuwa ni Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sisi tunasema kuwa ni kweli kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya hivo. Lakini tunawauliza; je, alifanya hivo akiwa imamu? Alifanya hivo akiswali peke yake. Mtu akiswali peke yake arefushe anavotaka kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini mtu akiwaswalisha watu anatakiwa kukhafifisha. Ni jambo linalotambulika kule imamu kutoa salamu kila baada ya Rakaa´ mbili ni kwepesi kwa watu kuliko kuzifululiza tano, saba au tisa. Hakuna Hadiyth hata moja kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Maswahabah Witr Rakaa´ tano, saba au tisa. Alikufanya akifanya hivo anaposwali peke yake. Sisi tunawaambia nyumbani mtu afanye Sunnah zote. Sisi tunashaji´isha mara mtu afanye hivi na mara nyingine abadilishe afanye vile kwa ajili ya kuhuisha Sunnah. Lakini kuwaswalisha hivo waislamu si sawa. Ikiwa kuna kundi maalum wamekubaliana kuswali Witr kwa Rakaa´ tano, saba au tisa kwa kufululiza ni sawa. Ama msikiti ambapo kila mmoja anakuja na kuswali imamu awaswalishe watu Rakaa´ mbili mbili.

Kuhusiana na kwamba watapomaliza kuswali Tarawiyh na imamu akasimama kuswali, wanatakiwa kunuia Witr. Haijalishi kitu hata kama ataswali Rakaa´ mbili kisha akatoa salamu bado ni Witr.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (41)
  • Imechapishwa: 30/05/2018