Sehemu za kupandisha mikono katika swalah


Swali: Je, ni wajibu kupandisha mikono wakati wa Takbiyrat-ul-Ihraam tu au ni lazima kuipandisha katika nguzo zote za Swalah?

Jibu: Sunnah ni kupandisha mikono wakati wa Ihraam, na wakati wa Rukuu´, na wakati wa kutoka katika Rukuu´ na wakati wa kusimama kutoka katika Tashahhud ya kwanza mpaka ya tatu. Na hilo sio wajibu bali ni Sunnah. Lilifanywa na Mtume (´alayhi-Salaam), Makhalifah waongofu na lilinukuliwa kutoka kwa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sunnah ni muumini mwanaume na mwanamke afanye hivyo katika Swalah zake zote. Kwa kuwa asli ni kuwa, mwanamke ni sawa na mwanaume katika Ahkaam isipokuwa kwa yale yaliyokhusishwa na dalili. Sunnah ni kunyanyua mikono yake katika Takbiyrah ya kwanza mpaka kwenye mabega au masikio yake, hali kadhalika (apandishe) mikono yake wakati wa Rukuu´ na wakati wa kuinuka kutoka katika Rukuu´, na hali kadhalika wakati wa kuinuka kutoka katika Tashahhud ya kwanza mpaka ya mwisho. Kama ilivyokuja katika khabari zilizo sahihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na hili ni jambo Mustahabah na Sunnah na sio wajibu. Na lau ataswali bila ya kupandisha, Swalah yake ni sahihi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Nuur ´alaad-Darb (770)
  • Imechapishwa: 15/03/2018