Ni lazima kuamini kuwa Muhammad ndiye mja na Mtume wa Allaah, yeye ndiye Nabii wa mwisho, yeye ndiye mbora katika Manabii, ametumwa na Allaah kwa waarabu na wasiokuwa waarabu na majini na watu. Asiyeamini hili ni kafiri na sio muumini hata kama atadai kuwa anampwekesha na kumuabudu Allaah.

Shahaadah mbili moja wapo haisihi isipokuwa mpaka kwa kupatikana nyingine. Mwenye kushuhudia ya kwamba hapana mola wa haki isipokuwa Allaah pasina kushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah, basi shahaadah yake haikubaliwi. Vilevile yule mwenye kushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah pasina kushuhudia kuwa hapana mola wa haki isipokuwa Allaah, shahaadah yake haikubaliwi. Ni lazima kupatikane shahaadah zote mbili. Kukitajwa moja [katika maandiko] iliyotajwa inaingia katika hiyo nyingine. Zikikutana zote mbili kwa wakati mmoja, shahaadah ya kwanza inafasiri kuwa ni kumpwekesha Allaah na ya pili inafasiriwa kuwa ni kushuhudia ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa ajili hii ndio maana Allaah amewakanushia imani Ahl-ul-Kitaab ambao ni mayahudi na manaswara kwa kuwa hawakushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah. Haijalishi kitu hata kama wanadai kuwa wanamwamini Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema katika Suurah “at-Tawbah”:

قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَن يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ

“Piganeni na wale wasiomwamini Allaah na wala Siku ya Mwisho, na wala hawaharamishi Aliyoyaharamisha Allaah na Mtume Wake, na wala hawafuati Dini ya haki miongoni mwa wale waliopewa Kitabu, [piganeni nao] mpaka watoe kodi kwa khiyari na hali ni madhalili.” (09:29)

Amewakanushia imani kwa kuwa wamekataa kumwamini Muhammad kuwa ni Mtume wa Allaah. Haijalishi kitu hata kama wao wanadai kuwa wanamwamini Allaah na wanatendea kazi Vitabu vyao. Lakini hata hivyo imani hii imekanushwa kwao na haisihi na inatupiliwa mbali.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/119-120)
  • Imechapishwa: 31/05/2020