Kuhusiana na dalili za Ahl-us-Sunnah juu ya kuthibitisha kuwa Allaah ataonekana Aakhirah wamesema kuwa kuonekana ni kitu kilichopo na hakihusiani isipokuwa na kitu kilichopo. Ambaye ana ukamilifu kwa kuwepo Kwake ana haki zaidi ya kuonekana kuliko chengeni. Kitu kinacholiweka hilo wazi zaidi ni kwamba kukosa kuonekana kwa kitu kunatokamana na moja kati ya sababu zifuatazo:

1- Kufichikana kile chenye kuonekana.

2- Udhaifu wa yule muonaji.

Allaah (Ta´ala) hakufichikana. Yeye yuwazi kuliko vitu vingine vyote vilivyopo. Kukosa kuonekana Kwake duniani kunatokamana na udhaifu wa kuona. Siku ya Qiyaamah waumini watapewa maumbile yenye viungo na macho yenye nguvu kabisa ambapo wataweza kwa maumbile hayo kumuona Allaah Aakhirah. Kuhusiana na duniani hawawezi kumuona Allaah kutokana na udhaifu wa uanaadamu wao. Ndio maana pale Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuomba kumuona Mola Wake Akamjibu kwa kusema:

لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي

“(Lan) Hutoniona! Lakini tazama jabali. Likitulia mahali pake, basi utaniona.” (07:143)

Alipojionyesha kwenye mlima ukavurugika na Muusa akaanguka chini hali ya kuwa ni mwenye kuzimia.

Ikiwa mtu hapa duniani hawezi kulitazama jua kwa kulikodolea macho ilihali jua ni kiumbe, vipi basi itawezekana kuonekana kwa Allaah [hapa duniani]? Bali mwanaadamu hawezi hata kumuona Malaika kwa umbile lake la asli isipokuwa ikiwa kama Allaah atampa uwezo huo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَوْ جَعَلْنَاهُ مَلَكًا لَّجَعَلْنَاهُ رَجُلًا

“Na lau Tungelimfanya Malaika, bila shaka Tungelimfanya [afanane kama] mtu.” (06:09)

وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ مَلَكٌ ۖ وَلَوْ أَنزَلْنَا مَلَكًا لَّقُضِيَ الْأَمْرُ

“Wakasema: “Mbona hakuteremshiwa Malaika?” Na lau Tungeliteremsha Malaika, basi ingepitishwa amri.” (06:08)

bi maana angelikufa. Mwanaadamu hawezi kumuona Malaika kwa umbile lake.

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona Malaika katika umbile lake la mara ya kwanza alishikwa na woga mkubwa na akaenda kwa mke wake na kumwambia:

“Nifunikeni! Nifunikeni!”

Lakini hata hivyo Allaah akawa amemfanya kuwa na nguvu. Ikiwa mwanaadamu hawezi kumuona Malaika katika umbile lake na jua kwa kulikodolea macho, vipi basi ataweza kumuona Allaah duniani? Lakini Aakhirah Allaah atawafufua wakiwa na maumbile yenye nguvu na wataweza kumuona Allaah (´Azza wa Jall).

Hizi ndio dalili za Ahl-us-Sunnah kutoka katika Qur-aan, Sunnah, maafikiano na akili juu ya kuthibitisha kuwa waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (01/230-231)
  • Imechapishwa: 30/05/2020