Unafiki na uzandiki unapatikana zaidi kwa Raafidhwah kuliko pote lingine lolote. Bali uhakika wa mambo ni kwamba ni lazima kila mmoja katika wao awe na chembechembe za unafiki. Kwani msingi wa unafiki ni uongo na mtu akasema kwa mdomo wake kile asichokiamini moyoni mwake. Kama Allaah alivyoeleza kuhusu wanafiki kwamba wanayasema mambo kwa ndimi zao wasiyoyaamini ndani ya nyoyo zao.

Raafidhwah wanafanya jambo hili kuwa ni moja katika misingi ya dini yao. Wanaita kitu hicho kuwa ni “Taqiyyah”. Wanainasibisha kwa maimamu wa Ahl-ul-Bayt, kitu ambacho Allaah amewatakasa nacho. Mpaka wamesikia kusema kwamba Ja´far as-Swaadiq amesema:

“Taqiyyah ni dini yangu na dini ya mababu zangu.”[1]

Allaah amewatakasa waumini katika Ahl-ul-Bayt na wengineo kutokamana na kitu kama hicho. Bali walikuwa miongoni mwa watu waaminifu na wenye dini zaidi. Dini yao ilikuwa ni kumcha Allaah (Taqwaa) na sio Taqiyyah. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِلَّا أَن تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً

”Isipokuwa mkiwa mnajilinda na shari zao.” (Aal ´Imraan 03:28)

Hapa kuna maamrisho ya mtu kujikinga dhidi ya makafiri, na sio unafiki na uongo. Allaah (T´ala) ameruhusu kwa yule ambaye ametenzwa nguvu kutamka maneno ya kufuru midhali moyo wake umetua juu ya imani. Hata hivyo hakuna yeyote katika Ahl-ul-Bayt aliyetenzwa nguvu kwa chochote katika hayo. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) hakumlazimisha yeyote si katika wao wala katika wengine kula kiapo cha utiifu kumpa yeye seuze kuwalazimisha kumsifu na kumtapa. Bali ´Aliy na wengineo katika Ahl-ul-Bayt walikuwa wakitaja fadhilah za Maswahabah waziwazi, wakiwasifu, wakiwatakia rehema na kuwaombea du´aa. Kuna maafikiano juu ya kwamba hakuna yeyote aliyewalazimisha kwa chochote katika hayo.

[1] al-Kaafiy (2/219) ya al-Kulayniy.

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhaaj-us-Sunnah an-Nabawiyyah (2/46-47)
  • Imechapishwa: 18/02/2019