Njia waliyoona kutumia maadui wa Uislamu ili kuwafarikisha waislamu


Baadhi ya makundi ya waislamu, kama Mu´tazilah, baadhi ya Ibaadhiyyah, Zaydiyyah na wengineo yamekubali fikira hizo – yaani za kupinga majina na sifa za Allaah – zilizopinda kabisa kutokamana na Qur-aan na Sunnah. Allaah aliukusanya Ummah kupitia viwili hivyo baada ya kufarikiana, kutawanyika, kuchukiana na wakawa makundi kwa makundi. Amesema (Ta´ala):

وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا

“Ikumbukeni neema ya Allaah juu yenu pale mlipokuwa maadui halafu Akaunganisha nyoyo zenu na mkawa kwa neema Yake ndugu.”[1]

Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimekuacheni vile ambavyo iwapo mtashikamana navyo basi hatompotea kabisa baada yangu: Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”[2]

Maadui wa Uislamu wakatambua kuwa kukusanyika kwa Ummah wa Kiislamu juu ya kuamini Kitabu cha Mola wake na Sunnah za Mtume wake na kushikamana navyo barabara ndio sababu kubwa ya utukufu, ushindi na kurudi kwa furaha yake. Ndipo wakaona hebu wawaingizie waislamu fikira zilizopinda katika mlango wa majina na sifa za Allaah na wakazieneza nyuma ya pazia eti ya kumtakasa Allaah (´Azza wa Jall) na kushabihiana na viumbe wake. Miongoni mwa sifa walizokanusha ni sifa ya kuzungumza kwa Allaah (´Azza wa Jall). Wakasema kuwa maneno hayatokamani isipokuwa kwa kuwepo ulimi, midomo na kwamba hii ni sifa ya viumbe na kwamba eti endapo watamthibitishia Allaah sifa ya kuzungumza basi watakuwa wamemfananisha na viumbe wake na kwamba yule mwenye kumfananisha Allaah na viumbe wake amekufuru.

Pindi baadhi ya waislamu, kama vile Mu´tazilah, Zaydiyyah, baadhi ya Ibaadhiyyah na wale wenye kudai Uislamu kama vile Raafidhwah, walipozikubali fikira hizo potevu – huenda wengine masikini hawajui propaganda za waliofanya hivo – ndipo maadui wa Uislamu wakayafikia malengo yao ambayo ni kuchochea fitina na kuutawanyisha Ummah. Hivyo ndivyo alivyosema al-Khaliyliy ambaye na yeye ametumbukia katika mtego huo.

[1] 03:103

[2] ad-Daarimiy (04/245) nambari. 149.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 189-190
  • Imechapishwa: 14/01/2017