Swali: Ni ipi hukumu ya wanaume kupiga makofi katika minasaba na sherehe?

Jibu: Kupiga makofi katika sherehe ni katika matendo ya kipindi cha kikafiri. Dogo liwezalo kusemwa ni kuwa imechukizwa. Udhahiri wa dalili zinaonyesha kuwa ni haramu. Kwa kuwa waislamu wamekatazwa kujifananisha na makafiri. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu sifa ya makafiri wa Makkah:

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً

“Na haikuwa swalaah zao katika Nyumba isipokuwa ni miluzi na kupiga makofi.”[1]

Wanachuoni wamesema kwamba kunamaanishwa kupiga firimbi na makofi.

Sunnah kwa muumini pindi anapoona au anaposikia yanayomshangaza ni yeye aseme:

سبحان الله

“Ametakasika Allaah.”

au aseme:

الله أكبر

“Allaah ni mkubwa.”

Hivyo ndivyo ilivyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth nyingi.

Kupiga makofi kumesuniwa kwa wanawake khaswa pindi wanapotaka kuzindua jambo katika swalah au wako pamoja na wanaume na imamu akawa amesahau kitu. Katika hali hii imesuniwa kwao kuzindua kwa kupiga makofi. Kuhusu wanaume wao wanatakiwa kuzindua kwa kusema:

سبحان الله

“Ametakasika Allaah.”

Hivyo ndivyo Sunnah ilivyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa haya inapata kutambulika kwamba wanaume kupiga makofi kuna kujifananisha na makafiri na wanawake. Yote mawili yamekatazwa.

[1] 08:35

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/151)
  • Imechapishwa: 02/07/2017