Nasaha na mwongozo kwa vijana wakati wa kulingania


Swali: Tunawaona vijana wengi wenye shauku ya kukataza maovu. Lakini hata hivyo hawafanyi vyema katika kukataza. Ni zipi nasaha na maelekezo yako kwa watu hao? Ni ipi njia bora ya kukemea maovu?

Jibu: Nasaha zangu kwao ni kwamba wahakikishe juu ya jambo na wasome ili wawe na uhakika kuwa jambo fulani ni mema au maovu kwa mujibu wa dalili ya Shari´ah ili jambo lao la kukemea liwe limetokana na utambuzi. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata. Utakasifu ni wa Allaah na mimi si miongoni mwa washirikina.”[1]

Aidha nawanasihi kukemea kwao kuwe kwa upole, maneno mazuri na njia nzuri ili waweze kukubaliwa na ili pia waweze kutengeneza zaidi kuliko watavyoharibu. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[2]

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu wangelikukimbia.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule ambaye atanyimwa upole basi hakika amenyimwa kheri zote.”

“Hakika upole hauwi kwenye kitu isipokuwa hukipamba na hauondoshwi kutoka kwenye kitu isipokuwa hukifanya kibaya.”

Zipo Hadiyth nyenginezo juu ya mada hii ambazo ni nyingi na Swahiyh.

Miongoni mwa mambo yanayotakikana kwa ambaye analingania kwa Allaah na mwenye kuamrisha mema na kukataza maovu ni kwamba anapaswa awe msitari wa mbele kabisa katika yale anayoamrisha na awe mtu wa mbali kabisa katika yale anayokataza ili asije kufanana na wale ambao Allaah amewasema vibaya pale aliposema (Subhaanah):

أَتَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبِرِّ وَتَنسَوْنَ أَنفُسَكُمْ وَأَنتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

“Je, mnaamrisha watu wafanye mema na mnajisahu nafsi zenu na hali ya kuwa nyinyi mnasoma Kitabu; je, hamtii akilini?”[4]

Amesema tena (Subhaanahu wa Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ

“Enyi walioamini!  Kwanini mnasema yale msiyoyafanya? Ni chukizo kubwa kabisa mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya.”[5]

Lengo jengine ni kwamba ili awe mwenye kumwingiliza katika jambo hilo na watu wanufaike kwa maneno na vitendo vyake.

[1] 12:108

[2] 16:159

[3] 03:159

[4] 02:44

[5] 61:02-03

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/74)
  • Imechapishwa: 28/01/2021