Nasaha kwa wazazi wenye kuipa kipaumbele dunia mbele ya Aakhirah juu ya watoto wao

Swali: Baadhi ya wazazi hawatilii umuhimu juu ya watoto kuhusiana na mambo ya dini. Kwa mfano utamkuta mzazi hamwamrishi mwanae kuswali, kusoma Qur-aan na kutangamana na watu wema. Lakini wakati huohuo utamkuta mzazi anaamrisha kuchunga masomo na anakasirika pindi mtoto anapokwepa. Ni zipi nasaha zako?

Jibu: Nasaha zangu kwa akina baba, maami na ndugu wengine wamche Allaah juu ya wale watoto walio na usimamizi juu yao na waamrishe kuswali pindi wanapofikisha miaka saba na wawapige kwayo wanapofikisha miaka kumi kama Hadiyth ilivyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofikisha miaka sana, wapigeni kwayo wanapofikisha miaka kumi na muwatenganishe kwenye malazi.”

Kwa hivyo ni lazima kwa akina baba, kina mama na ndugu wengine wawasimamie wale wenye kuwaongoza kuhusiana na jambo la swalah na mengineyo na wawazuie kutokamana na yale aliyoharamisha Allaah na wawalazimishe yale aliyowajibisha Allaah. Huu ndio wajibu. Wao ni amana kwao. Allaah (Subhaanah) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا

“Enyi walioamini! Ziokoeni nafsi zenu na familia zenu kutokamana na moto.”[1]

وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا

“Amrisha ahli zako swalah na dumisha kusubiri kwayo.”[2]

Amesema kuhusu Nabii na Mtume Wake Ismaa´iyl (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِسْمَاعِيلَ ۚ إِنَّهُ كَانَ صَادِقَ الْوَعْدِ وَكَانَ رَسُولًا نَّبِيًّا وَكَانَ يَأْمُرُ أَهْلَهُ بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ وَكَانَ عِندَ رَبِّهِ مَرْضِيًّا

”Mtaje katika Kitabu Ismaa’iyl. Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Mtume na Nabii na alikuwa akiwaamrisha ahli zake swalah na zakaah na alikuwa mridhiwa mbele ya Mola wake.”[3]

Kwa hiyo ni lazima kwetu kutekeleza amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwalazimisha wake zetu na watoto wetu kumtii Allaah na kumtii Mtume Wake juu ya jambo la swalah na mengineyo. Sambamba na hilo tuwazuie dhidi ya yale aliyokataza Allaah na Mtume Wake kama kwa mfano kuacha swalah, kunywa pombe, kuvuta sigara, kusikiliza ala za pumbao, kutangamana na marafiki waovu na mengineyo na tuwalazimishe kutangamana na marafiki wema. Haya ndio ya lazima kwa wale wasimamizi juu ya wale wavulana na wasichana anaowasimamia. Allaah (Subhaanah) atawauliza juu ya hayo siku ya Qiyaamah. Amesema (Subhaanah):

فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Basi naapa kwa Mola wako  bila shaka Tutawauliza wote juu ya yale waliyokuwa wakitenda.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nyote ni wachungaji na nyote mtaulizwa juu ya kile mlichokichunga. Mwanaume ni mchungaji kwa familia yake na ataulizwa juu yao. Mwanamke ni mchungaji na ataulizwa juu ya nyumba ya mumewe. Mtumwa ni mchungaji juu ya mali ya bosi wake na ataulizwa juu ya kile alichochungishwa.”

[1] 66:06

[2] 20:132

[3] 19:54-55

[4] 15:92-93

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (07/184) https://binbaz.org.sa/fatwas/2031/%D9%86%D8%B5%D9%8A%D8%AD%D8%A9-%D9%84%D9%84%D8%A7%D8%A8%D8%A7%D8%A1-%D8%A7%D9%84%D8%B0%D9%8A%D9%86-%D9%8A%D9%87%D8%AA%D9%85%D9%88%D9%86-%D8%A8%D8%A7%D9%85%D9%88%D8%B1-%D8%A7%D9%84%D8%AF%D9%86%D9%8A%D8%A7-%D8%B9%D9%86-%D8%A7%D9%84%D8%AF%D9%8A%D9%86
  • Imechapishwa: 22/11/2019