Mzazi kusafiri kwenda Makkah na kuiacha familia yake inazorota


Swali: Ni ipi hukumu ya ambaye anaenda na familia yake Makkah kufanya ´Umrah na anawaacha watoto wake kuzurura barabarani na wala yeye haswali. Hata hata mwanamke wake anazurura masokoni kati ya wanaume na yeye yuko Haram anaswali. Lakini hata hivyo hawajali. Je, mtu huyu ni mwenye kupata thawabu au dhambi?

Jibu: Nasema kujengea juu ya imani iliyojengwa juu ya msingi: ya kwamba ni mwenye kupata dhambi na hapati thawabu. Kwa nini? Kwa sababu ameacha jambo ambalo Allaah amembebesha nalo kwa kufanya jambo ambalo sio la wajibu. Ni kipi alichombebesha Allaah? Kuiangalia familia yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا

“Enyi walioamini! Ziokoeni nafsi zenu na familia zenu kutokamana na moto.” (66:06)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanaume ni mchungi juu ya familia yake na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.”

Ni matahadharisho gani Allaah (´Azza wa Jall) anatupa ya kuziokoa nafsi zetu na familia zetu kutokamana na Moto na ni majukumu yepi ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu´alayhi wa sallaam) ametupa na huku eti mtu anakaa kwenye msikiti Mtakatifu pamoja na uzito, dhiki, kuwaangalia wanawake na mambo mengine anayokumbana nayo. Sambamba na hilo amewaacha watoto wake – wakiume na wakike – wanatangatanga masokoni. Uangalizi uko wapi? Amana iko wapi? Nasema kuwa anapata dhambi. Endapo atasema: “Ikiwa napata dhambi kwa kwenda na familia yangu basi ni bora ni waache katika nchi yangu na nende mimi peke yangu.” Tunamwambia ni sawa. Lakini tunamuuliza: “Ukiwaacha familia yako nchini mwako wana mtu wa kuwaangalia?” Akijibu ndio, basi tunamwambia ni sawa na hapo wewe unaweza kwenda. Kwa sababu kwenda kwake hakupelekei katika madhara yoyote na hakutopatikana mapungufu kwa familia yake wala hatokuwa ametumia vibaya amana alopewa. Lakini endapo atajibu kwamba akisafiri hawana yeyote wa kuwaangalia na kutatokea ujinga mwengine, basi tunamwambia asende na wala hakuna kufanya ´Umrah. Isipokuwa ikiwa kama ataweza kusafiri kwa ndege mwanzoni mwa mchana na kurudi kwa ndege mwishoni mwa mchana. Kufanya hivi ni kwa sababu asipoteze wakati juu ya kuiangalia familia yake.

Mimi nasema hali ya kuwa ni amana ninayoifikisha kwa yule anayemtaka Allaah: dini haiendi kwa hisia. Dini inaenda kwa mujibu wa mipaka na Shari´ah zilizowekwa na Allaah (´Azza wa Jall). Tazama matendo yako kabla ya kufanya yale yanayotamaniwa na nafsi yako. Je, matendo yako yanaendana na Shari´ah au hapana? Ikiwa yanaendana na Shari´ah basi hizo ni fadhila za Allaah. Unachotakiwa ni wewe kufanya yale yanayoendana na Shari´ah. Ingelikuwa dini inaendana na hisia basi Ahl-ul-Bid´ah wote wangelikuwa wangelikuwa juu ya haki. Kwa sababu haya ndio ambayo hisia zao zinakopelekea.

Suufiyyah wanaonelea kuwa wao ndio wako katika kiwango cha juu kabisa cha imani.

Mu´attwilah wanaomkanushia Allaah majina na sifa wanaonelea kufanya hivo ndio kiwango cha juu kabisa cha kumtakasa Allaah.

Mumaththilah wanaozifananisha sifa na majina ya Allaah wanaonelea kufanya hivo ndio kiwango cha juu kabisa cha kufananiza.

Lakini hata hivyo dini ni Shari´ah zilizowekwa kutoka kwa Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mambo yakiwa ni hivo basi kila kinachoingia kwenye bongo lako kinakuwa ni Shari´ah. Haya ni sahihi. Washirikina pindi wanaposhirikisha inakuwa ni matamanio yao au ni kufuata Shari´ah? Ni kufuata matamanio yao. Wao wanasema:

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah.” (39:03)

Je, tuseme kuwa ni haki? Kule mtu kufanya kwa mujibu wa matamanio yake na yale anayohisi na kuonelea kuwa ndio Shari´ah na kuyapa mgongo yale Allaah aliyomuwajibishia ni kosa kubwa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ

”Lau kama haki ingelifuata matamanio yao, basi zingeliharibika mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Bali Tumewaletea ukumbusho wao lakini wao ni wenye kupuuza ukumbusho wao.” (23:07)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (33) http://binothaimeen.net/content/738
  • Imechapishwa: 10/11/2017