Mume kumwaga manii nje ya tupu ya mke wake


Swali: Ni sahihi kwa mwanaume kumuosha mke wake anapokufa au msichana wa mwaka moja mpaka miwili hata kama atakuwa ni ajinabi kwake?

Jibu: Hakuna ubaya wowote mwanaume kumuosha mke wake, na mke kumuosha mume wake kwa kufuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama kinyume na mke, hapana. Lakini mdogo ni kama mfano wa mke. Hakuna ubaya mwanaume akamuosha msichana mdogo, na wala hakuna neno akamuosha kama mke. Ama mama yake, msichana wake, dada yake na mfano wa hao, haifai kwake kuwaosha. Bali hawa wanaoshwa na wanawake. Lakini msichana ambaye ni mdogo haina neno anaweza kuoshwa na wanaume. Ikiwa ni chini ya miaka saba; kama mfano wa msichana wa miaka mitano, tatu, mine, haina neno. Hali kadhalika, mvulana wa chini ya miaka saba anaweza kuoshwa na wanawake pia. Watoto chini ya miaka saba wanaweza kuoshwa na wanaume na wanawake.

Swali: Mwanaume aliyeoa kumwaga manii nje ya tupu ya mwanamke ni haramu au hapana? Na khaswa anafanya hivi wakati wa hali ya hedhi au damu ya uzazi?

JIbu: Kumwaga manii nje ya tupu ikiwa kuna manufaa, hakuna neno kufanya hivyo. Na hii huitwa “´Azl”. Na imethibiti ya kwamba Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakifanya ´Azl, na akawakubalia hilo (´alayhis-Swalaat was-Salaam). Kukiwa na haja ya kufanya ´Azl, bi maana kumwaga manii yake nje ya tupu, ima kwa kuwa mke wake hawezi kushika mimba nyingine wakati ule au kwa sababu aliyoisema muulizaji. Kwa kuwa lililo la haramu (wakati wa hedhi na nifasi) ni kufanya nae jimaa. Akicheza nae katika tupu yake (mke) na akamwaga manii kwa nje na wala asimjamii, hakuna ubaya kufanya hivyo. Kwa kuwa haramu ni kufanya jimaa. Kasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na mwanamke wa hedhi: “Fanya kila kitu isipokuwa (kitendo cha) ndoa.” Yaani jimaa. Anaweza kukutana nae, kumkumbatia, kucheza nae na kustarehe nae kwa tupu yake, tumbo lake na yasiyokuwa hayo. Lakini bora zaidi, awe na kizuizi kwa juu kama ´Izaar au suruwaliili kujiepusha na khatari. Kwa kuwa mwenye kuikabili tupu, Shaytwaan anaweza kumshawishi kufanya kitendo cha jimaa kilochoharamishwa. Bora, ni yeye (mume) akutane nae nyuma ya ´Izaar, suruwali au kanzu. Anasema ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha):

“Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiniamuru nijifunge vizuri nguo yangu kiunoni kisha akinikumbatia hata nikiwa katika hedhi.”

Namna hii ndivyo alivyosema ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha). Makusudio ni kuwa, Sunnah kwa upande wa mume ikiwa mwanamke yuko katika hedhi au nifasi, akutana nae nyuma ya ´Izaar au nyuma ya suruwali na mfano wa hivyo. Lakini lau akikutana nae ndani ya ´Izaar na ndani ya suruwali, hakuna ubaya wa hili. Kumekuja katika Sunnah kitu kinachotolea dalili hilo. Kwa kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fanya kila kitu isipokuwa (kitendo cha) ndoa.”

Ilikuwa ni baada ya kuambiwa kuwa mayahudi pindi mwanamke anapoingia hedhini, basi wanamchukia, wanamtenga na kumhama nyumbani. Ndio akawa amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fanya kila kitu isipokuwa (kitendo cha) ndoa.”

Yaani wakhalifuni mayahudi, bi maana fanya kila kitu ila jimaa. Hivyo akiweka tupu yake kwenye mapaja na akaweka nje ya tupu, hakuna ubaya. Lakini asimjamii, ni haramu kwake kumjamii sawa ikiwa atateremsha au kutoteremsha. Ni wajibu kujiepusha na jimaa. Ama kule kuweka kwake tupu yake kwenye mapaja yake au karibu na tupu yake (mke) mpaka akamwaga bila ya kuiingiza, hakuna ubaya kwa hilo. Lakini lililo bora zaidi kabisa, ni yeye kujiepusha na hili, ili Shaytwaan asimshawishi kufanya kitendo kilichoharamishwa. Na kwa ajili ya hili, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kawaamrisha wanawake wajisitiri (tupu zao) wakati wa kukutana nao moja kwa moja (´alayhis-Swalaat was-Salaam).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Nuur ´alaad-Darb
  • Imechapishwa: 17/03/2018