Mume aliyefunga amemwingilia mke wake wakati wa hedhi

Swali: Siku moja wapo ya Ramadhaan mume wangu aliniingilia mchana wa Ramadhaan ilihali niko na hedhi na yeye amefunga. Ni ipi hukumu?

Jibu: Swali hili limekusanya mambo mawili:

La kwanza: Ya kwamba mume huyu amemwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan. Ni wajibu kwake kulipa siku hiyo pamoja na kutoa kafara. Vilevile ni wajibu kwake kutubu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Anatakiwa kulipa siku badala ya ile ambayo amemwingilia ndani yake.

Kuhusu kafara anatakiwa kuachia mtumwa huru, asipopata anatakiwa kufunga miezi miwili mfululizo, asipoweza anatakiwa kulisha masikini sitini.

Kuhusu uwajibu wa kulipa ni kutokana na yale yaliyopokea Ibn Maajah kwa mlolongo wake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia yule bedui aliyemwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan:

“Funga siku badala yake.”[1]

Kuhusu uwajibu wa kutoa kafara ni kutokana na yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika “as-Sunan” na kwenginepo ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia yule bedui ambaye alimwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan:

“Achie mtumwa huru.” Akasema: “Sina.” Akamwambia: “Funga miezi miwili mfululizo.” Akasema: “Siwezi.” Akamwambia: “Walishe masikini sitini.”[2]

Ama mwanamke haimlazimu kitu. Kwa sababu uwajibu wa kufunga umeanguka kwa yule mwenye hedhi.

La pili: Amemwingilia mke wake akiwa na hedhi. Ni wajibu kwake kutoa dinari au nusu ya dinari kutokana na Hadiyth ya Ibn ´Abbaas:

“Atoe dinari au nusu yake.”[3]

Ameipokea Ahmad, at-Tirmidhiy na Abu Daawuud. Amesema kuwa mapokezi mengine Swahiyh yanasema hali kadhalika.

Makusudio ya dinari ni vipande cha dhahabu au fedha ilio na thamani yake.

Ikiwa mwanamke huyu alifanya hali ya kupenda na yeye pia anatakiwa kutoa kafara kama mwanaume na wote wawili wanatakiwa kutubu kwa Allaah (Subhanaah) kwa kufanya jimaa wakati wa hedhi.

[1] Ibn Maajah (1671) na Ahmad (02/208).

[2] at-Tirmidhiy (3299), Abu Daawuud (2213), Ibn Maajah (2062), Ahmad (05/436) na ad-Daarimiy (2273).

[3] Ahmad (01/230), Abu Daawuud (01/181-183) na wengineo.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (10/304-305)
  • Imechapishwa: 14/06/2017