Mtu wa kwanza kuzungumza juu ya Fiqh-ul-Waaqi´ leo

Jambo hili – yaani Fiqh-ul-Waaqi´ (uelewa wa kisasa) – ni jipya. Kutokana na ninavyojua mtu wa kwanza kulizungumza leo ni Sayyid Qutwub katika kitabu chake “Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan” katika Suurah “Yuusuf” katika mnasaba wa maneno ya Allaah (Ta´ala):

قَالَ اجْعَلْنِي عَلَىٰ خَزَائِنِ الْأَرْضِ ۖ إِنِّي حَفِيظٌ عَلِيمٌ

“Akasema: “Niweke nisimamie hazina ya nchi, hakika mimi ni mhifadhi mjuzi.”” (12:55)

Hapa akagawa uelewa sehemu mbili; uelewa wa makaratasi na uelewa wa kiharakati. Akasema kuwa uelewa wa kiharakati umejengwa juu ya uelewa wa kisasa. Akasema kuwa ni lazima harakati, bi maana ni lazima juu ya chama za Kiislamu kitilie umuhimu uelewa wa kisasa kwa sababu harakati zimejengwa juu yake. Akaupa kipaumbele uelewa wa kisasa juu ya kile anachokiita kuwa ni uelewa wa makaratasi. Amesema kuwa uelewa wa makaratasi, ambao ni uelewa wa Qur-aan na Sunnah, unahitajika baada ya kuwa nchi ya Kiislamu imeshasimamishwa. Ni vipi mtu atatilia umuhimu uelewa wa makaratasi ikiwa nchi ya Kiislamu au jamii ya Kiislamu haina nguvu za kisiasa zilizoshinda? Kwa hiyo, anasema, kujishughulisha na uelewa wa makaratasi kutakuwa hakuna maana yoyote usiyoweza kutumiwa katika hali fulani. Kisha akatilia mkazo juu ya uelewa wa kisasa. Kutokana na ninavyojua yeye ndiye wa kwanza aliyefanya mgawanyo huu na kuyasema hayo.

Mtu wa kwanza kutamka fikira hizi ni Sayyid Qutwub. Alijenga hilo juu ya mtazamo usiokuwa wa sawa unaosema kuwa uelewa wa Qur-aan na Sunnah hauhitajiki isipokuwa baada ya kusimama nchi ya Kiislamu. Hili ni kosa. Da´wah ambayo haikujengwa juu ya uelewa wa Qur-aan na Sunnah katika nchi isiyokuwa ya Kiislamu haiunufaishi Uislamu kitu. Bali Da´wah kama hiyo ni ya uzushi. Watu watilie mkazo kitu gani ikiwa uelewa haukujengwa juu ya Qur-aan na Sunnah?

  • Mhusika: Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://saleh.af.org.sa/sites/default/files/052.mp3
  • Imechapishwa: 09/08/2020