Imani sio kutambua ndani ya moyo kama wanavyosema Jahmiyyah. Madhehebu yao khabithi yanapelekea juu ya kwamba Fir´awn ni muumini. Kwa sababu alitambua kwa moyo wake [ukweli wa] yale aliyokuja nayo Muusa (´alayhis-Salaam):

قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ

“Hakika umekwishajua kwamba hakuna aliyeteremsha haya isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi.” (17:102)

Alikuwa akiyatambua haya kwa moyo wake. Lakini hata hivyo aliyakana kwa sababu ya kiburi tu na ili aweze kubaki juu ya ufalme wake. Hivyo ndio maana akawa ametilia jeuri yale aliyokuja nayo Muusa (´alayhis-Salaam).

Vilevile washirikina wanatambua kwa mioyo yao ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na kwamba yuko juu ya haki. Amesema (Ta´ala):

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ

“Kwa hakika Tunajua kuwa yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Hakika wao hawakukadhibishi wewe, lakini madhalimu wanakanusha Aayah za Allaah.” (06:33)

Wao si kwamba wanamkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kilichofanya kumkhalifu ni ukanushaji, kiburi, kuwa na jeuri juu ya haki na kasumba juu ya batili. Haya haya ndiyo yalifanya Abu Twaalib, ambaye ni ami yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alitambua kuwa Mtume ndiye yuko katika haki. Amesema:

Hakika nimejua kuwa dini ya Muhammad

ndio dini bora kabisa

Pindi alipokuwa si mwenye kumfuata na akafa juu ya mila ya ´Abdul-Muttwalib – ambayo ilikuwa juu ya shirki – akawa ni katika watu wa Motoni. Pamoja na kwamba alikuwa akitambua kuwa dini ya Muhammad ni haki. Amesema:

Lau si lamawa au kuchelea kutukanwa

basi mgeniona kwa hayo ni mwenye kujisalimisha waziwazi

Hakuna kilichomzuia kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa kuwa na mori juu ya dini za mababa na mababu zake. Mori ndio ukamzuia na matokeo yake akafa juu ya ukafiri. Vinginevyo anajua kuwa Muhammad yuko katika haki na anaamini hili. Kujengea juu ya madhehebu ya Ashaa´irah yanapelekea kwamba ni muumini.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Haa-iyyah, uk. 203-205
  • Imechapishwa: 18/02/2017