Mswaliji amesahau akasimama Rak´ah ya tatu katika Tarawiyh

Swali: Imamu akiswali Tarawiyh Rak´ah tatu kwa kujengea kwamba alikuwa anakusudia kuswali Rak´ah mbili. Je, katika Sunnah kumetajwa kwamba atasujudu sijda ya kusahau?

Jibu: Ndio, ipo sijda ya kusahau ikiwa alikuwa amekusudia kuswali Rak´ah mbili kawaida. Kwa sababu Sunnah juu ya swalah ya usiku ni Rak´ah mbilimbili. Akisimama katika Rak´ah ya tatu anatakiwa kuzindushwa kwa kuambiwa:

سبحان الله

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu.”

Katika hali hiyo atatakiwa kurudi na kukamilisha Tahiyyaat, kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuomba du´aa. Kisha asujudu sijda ya kusahau na kisha atoe salamu. Akipitiliza na asiketi chini atatakiwa kuzinduliwa mpaka aketi chini hata kama ni baada ya Rak´ah ya tatu. Anatakiwa kuketi chini, asome Tahiyyaat na yanayokuja baada yake katika kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuomba du´aa. Halafu asujudu sijda ya kusahau na kutoa salamu. Kama ambavo sijda ya kusahau imesuniwa katika swalah ya faradhi vivyo hivyo imesuniwa katika swalah ya sunnah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (16/30)
  • Imechapishwa: 06/05/2020