Hakika mlango wa majina na sifa za Allaah ni katika Aayah za Muhkam na zilizo wazi kabisa ambazo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wabingwa wa lugha ambao Qur-aan imeteremka kwa lugha yao walizipokea kwa kuzikubali na kujisalimisha halafu baada ya hapo wakaziamini na kuzitendea kazi na vilevile kumuomba Allaah masuala ya ´ibaadah na ya haja. Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖوَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ

”Allaah ana majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo. Waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake.”[1]

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameafikiana ya kwamba sifa za Allaah (´Azza wa Jall) ni katika Aayah za Muhkam ambazo maana yake inajulikana. Imaam Maalik amesema kuhusu kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi:

“Kulingana kunajulikana, namna haijulikani na kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah.”

Kinachotatiza ni namna yake na sio maana yake.

Kwa ajili hii haikuthibiti kutoka kwa Swahabah yoyote ya kwamba alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu jina au sifa yoyote ya Allaah. Hilo si kwa sababu nyingine isipokuwa ni kwa kuwa ni Muhkam na zilizo wazi maana yake. Dalili ya hilo ni kwamba Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) – ambao ndio watu wenye pupa zaidi katika Ummah juu ya kuitambua dini yao na khaswa katika yale mambo yanayohusiana na ´Aqiydah na juu ya yale ambayo ni wajibu kwao kuamini kuhusiana na Mola wao, Muumbaji wao na mwenye kuyaendesha mambo yao – waliuliza juu ya mambo mengi yaliyowatatiza na Allaah (´Azza wa Jall) akawaletea majibu. Kuna Aayah nyingi zimezokuja kwa tamko “wanakuuliza” kama mfano wa maneno Yake (Ta´ala):

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ

“Wanakuuliza kuhusu mvinyo na kamari.”

Jibu likaja:

قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا

“Sema: “Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na manufaa kwa watu – na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.””[2]

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَهِلَّةِ

“Wanakuuliza kuhusu miezi [inapoandama].”

Jibu likaja:

قُلْ هِيَ مَوَاقِيتُ لِلنَّاسِ وَالْحَجِّ

“Sema: “Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa watu na Hajj.””[3]

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَىٰ

”Wanakuuliza kuhusu mayatima.”

Jibu likaja:

قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ

“Sema: “Kuwatengeneza ni kheri.””[4]

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi.”

Jibu likaja:

قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ

“Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi.””[5]

Kama unavyoona mwenyewe kumekuja majibu kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) juu ya maswali hayo. Lakini hata hivyo hatukupata katika Qur-aan swali hata moja likiuliza jina au sifa yoyote miongoni mwa majina au sifa za Allaah. Hilo si kwa sababu nyingine ni kwa kuwa ziko wazi na maandiko yanaweka wazi maana yake.

[1] 07:180

[2] 02:219

[3] 02:189

[4] 02:220

[5] 02:222

  • Mhusika: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd al-Qawiym, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 13/01/2017