36. Msafiri amefika mjini mwake mchana wa Ramadhaan

Msafiri akifika katika mji wake mchana wa Ramadhaan hali ya kuwa amefungua basi swawm yake siku hiyo haikusihi. Kwa sababu alikuwa amefungua katikati ya mchana. Swawm ya lazima haisihi isipokuwa kuanzia kuchomoza kwa alfajiri.

Je, ni lazima kwake kujizuia siku iliobaki? Wanachuoni wametofautiana juu ya hilo. Wamoja wamesema kuwa ni lazima kwake kujizuia siku iliobaki kwa ajili ya kuheshimu zama na pia ni lazima kwake kuilipa kwa sababu haikusihi swawm ya siku hiyo. Maoni haya ndio yaliyotangaa katika madhehebu ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Wanachuoni wengine wakasema kuwa si lazima kwake kujizuia masaa yaliyobaki ya siku hiyo kwa sababu hafaidiki chochote kwa kujizuia huko kwa sababu baadaye atalazimika kuja kulipa. Heshima ya zama imeondoka kwa kula kwake alikoruhusiwa sehemu ya mwanzo ya mchana kwa waziwazi na kwa kujificha. ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mwenye kula sehemu ya mwanzo ya mchana basi ale sehemu yake ya mwisho.”

Hiyo ina maana kwamba yule ambaye imehalalika kwake kula sehemu ya mwanzo ya mchana kwa sababu ya udhuru basi itahalalika kwake kula sehemu yake ya mwisho. Haya ndio madhehebu ya Maalik, ash-Shaafi´iy na upokezi mmoja kutoka kwa Ahmad. Pamoja na hivo asifanye waziwazi kula na kunywa kwake kwa kufichika sababu ya kufungua na matokeo yake akajengewa dhana mbaya au watu wengine wakamwigiliza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 03/05/2020