Mfano wa namna mtu anavyoadhibiwa kwa kuwatukana wanachuoni

Swali: Kuna mmoja katika ndugu zetu vijana amekuwa na mfumo wa kukufurisha kiasi cha kwamba ikampelekea kuacha swalah ya mkusanyiko na akachukulia usahali heshima za watu. Tumemnasihi juu ya hayo na kuwatukana wanachuoni lakini hata hivyo haikufua dafu. Ni upi wajibu wetu juu ya mtu huyu na tumfanye nini?

Jibu: Huyu ameadhibiwa na tunaomba kinga kwa Allaah. Hii ni adhabu. Pindi alipokuwa ni mwenye kuwatukana wanachuoni na kuwadhulumu ndipo akapewa adhabu ya janga hili kwa njia ya kwamba anawakufurisha waislamu, amejitenga nao na ameacha kuswali misikitini kwa kuwa anaonelea kuwa ni makafiri. Huu ni msiba mkubwa. Namna hii ndivyo shari hupea kwa mtu kwa kuwa ni yenye kutoka kwa shaytwaan. Shaytwaan ndiye amempendezeshea kukufurisha na akamkuzia nayo mpaka akafikia kuwakufurisha waislamu wanaoswali misikitini, wanaadhini na wanakimu swalah. Hii ni adhabu.

Lakini hatukati tamaa ya kwamba Allaah atamwongoza na kumrudisha katika usawa. Ni juu yenu kumlingania katika dini ya Allaah na kumpa nasaha. Huenda Allaah akamwongoza. Isipokuwa ikiwa kama ni mpungufu wa akili. Katika hali hii itakuwa sio jambo kalifanya kwa khiyari yake. Bali ni kwa sababu amepungukiwa na akili na hivyo anachanganya mambo. Katika hali hii atakuwa na hukumu nyingine.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Furqaan (02) http://alfawzan.af.org.sa/node/2045
  • Imechapishwa: 12/10/2016