Maana ya Hadiyth “Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini… “

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe mwenye kunywa pombe pindi anapokunywa pombe hali ya kuwa ni muumini na wala haibi mwenye kuiba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini.”

Maana yake ni matishio na matahadharisho. Kwa msemo mwingine ni kwamba mtu huyo si mwenye imani kamilifu na kwamba imani yake ni pungufu. Haina maana kwamba ni kafiri. Kwa sababu Aayah na Hadiyth zinasadikishana. Kitabu cha Allaah hakikadhibishani. Sunnah hazipingani na Qur-aan. Kwa hivyo ni lazima kuyafasiri baadhi ya maandiko kwa maandiko mengine. Maneno yake:

“Hazini mwenye kuzini wakati anapozini hali ya kuwa ni muumini.”

Bi maana ile imani inayotakiwa ambayo ni kamilifu. Angelikuwa na imani kamilifu basi asingezini. Lakini imani yake ni pungufu na ndio maana akatumbukia ndani ya uzinzi na pombe kutokana na imani yake pungufu. Maana yake si kwamba ni kafiri. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha mzinzi asimamishiwe adhabu ya Kishari´ah. Adhabu hiyo inakuwa ndio kafara yake. Vivyo hivyo mnywa pombe anasimamishiwa adhabu ikiwa ndio kafara yake. Mzinzi akifa juu ya uzinzi baada ya kusimamishiwa adhabu anaingia Peponi na adhabu hiyo inakuwa ni kafara kwake. Kwa ajili hii Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema juu ya waja wema pindi alipotaja maasi:

“Yule ambaye Allaah atamsibu duniani – bi maana kwa kumsimamishia adhabu ya Kishari´ah – basi hiyo ndio kafara yake. Na yule ambaye Allaah atamcheleweshea huko Aakhirah, basi jambo lake liko kwa Allaah.”

Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.” (an-Nisaa´ 04:48)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (01/39)