Swali: Je, inasihi swalah ya anayeswali peke yake endapo atakuja mswaliji na akajiunga pamoja naye ambapo yeye akawa imamu wake?

Jibu: Ndio, swalah yao ni sahihi. Dalili ya hilo ni yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na Muslim ambapo Ibn ´Abbaas amesimulia kuwa alilala kwa shangazi yake Maymuunah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasimama kuswali usiku ambapo Ibn ´Abbaas akaja na kujiunga pamoja naye na akaendelea na swalah yake[1]. Hii ilikuwa swalah ya usiku. Kinachofaa katika swalah ya Sunnah kinafaa vilevile katika swalah ya faradhi midhali hakuna dalili. Hakuna dalili inayotofautisha kati ya swalah ya faradhi na ya sunnah katika masuala haya. Bali Imaam Ahmad amepokea kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaswali Maghrib. Nikaja na kusimama upande wake wa kushoto ambapo akaniweka upande wa kuliani mwake… “[2]

Hii ilikuwa swalah ya faradhi. Kuna wanachuoni wenye kuonelea kuwa kitendo hicho hakifai. Ni mamoja ni swalah ya faradhi au ya sunnah. Hayo ndio maoni yanayotambulika katika madhehebu [ya Hanaabilah]. Imesemekana vilevile kuwa inafaa katika swalah za sunnah na sio za faradhi.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Ahmad (03/326) na Ibn Maajah (974).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/447)
  • Imechapishwa: 23/07/2017