Kuvaa mapambo au nguo zilizo na majina ya Allaah au Aayah za Qur-aan

Swali: Mimi nina kicheni cha dhahabu na kimeandikwa juu yake jina la Allaah. Je, inafaa kukitumia au kitendo hicho ni haramu?

Jibu: Kicheni cha dhahabu ambacho kina jina la Allaah na pia kina Aayah miongoni mwa Aayah za Qur-aan inatakikana kukiacha. Kwa sababu mtu anaweza kuingia nacho chooni. Bora ni kukiacha. Mtu anaweza kukiweka sehemu dhalilifu. Bora ni wewe kukibadili kicheni hichi kwa njia ya kuondosha yale majina ya Allaah yaliyoko juu yake ili kisitwezwe. Majina ya Allaah ni matukufu. Kicheni kinaweza kuwekwa katika baadhi ya bidhaa, katika chumba na kwenye sanduku na mtu akakipuuza. Kicheni hicho kinaweza kuguswa na kitu kisichokuwa kizuri. Kwa kifupi ni kwamba bora ni kuacha na ni njia salama zaidi ya kuyatukuza majina ya Allaah (´Azza wa Jall).

Vivyo hivyo mavazi yanayokuwa na majina ya Allaah au Aayah za Qur-aan. Haijuzu kuvaa mavazi kama hayo. Kwa sababu ni njia inayopelekea kuyatweza au kupatwa na najisi kama mfano wa hedhi au najisi nyenginezo. Pia mavazi hayo yanaweza kukanyagwa na watu pindi anapoyaweka chini. Kwa ajili hiyo ni haramu kuyavaa, kuyafanya mito au kuyafanya mikeka. Kwa sababu vitu hivyo vinapelekea yakatweza kwa kuyakalia, kuyakanyaga na mfano wa mambo kama hayo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa ad-Duruus https://binbaz.org.sa/fatwas/7005/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D9%84%D8%A8%D8%B3-%D8%A7%D9%84%D8%AD%D9%84%D9%8A-%D8%A7%D9%88-%D8%A7%D9%84%D8%AB%D9%8A%D8%A7%D8%A8-%D8%A7%D9%84%D8%AA%D9%8A-%D8%B9%D9%84%D9%8A%D9%87%D8%A7-%D8%A7%D8%B3%D9%85-%D8%A7%D9%84%D9%84%D9%87
  • Imechapishwa: 11/05/2020