Swali: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ambaye ataiua nafsi yake kwa chuma, basi chuma chake kitakuwa mkononi mwake; atajichoma kwacho tumboni mwake ndani ya Moto wa Jahannam hali ya kuwa ni mwenye kudumishwa humo milele. Ambaye ataiua nafsi yake kwa sumu, basi sumu yake itakuwa mkononi mwake; atajipa sumu ndani ya Moto wa Jahannam hali ya kuwa ni mwenye kudumishwa humo milele. Ambaye atajirusha kutoka mlimani na akajua, basi atajirusha ndani ya Moto wa Jahannam hali ya kuwa ni mwenye kudumu humo milele.”[1]

Ni yepi makusudio ya kudumu milele? Je, kunamuhusu tu yule mwenye kujiua? Je, inafaa kumuombea rehema yule ambaye amejifanyia kitu kama hicho?

Jibu: Hili ni swali muhimu sana. Wakati mwingine inakuja ndani ya Qur-aan na Sunnah elimu inayofungua matarajio, kukiwemo namna ambavo matendo mema yanafuta madhambi, yanapelekea kuingia Peponi na mfano wa hayo. Watu wenye matarajio makubwa kuliko khofu hufurahikia elimu kama hizo na hivyo wakaanza kuyachukulia wepesi maasi. Huu ni ufahamu wa kimakosa juu ya maandiko ya matarajio. Upande wa pili yanakuja maandiko mengine yanayotaja matokeo ya madhambi, ikiwa ni pamoja na kwamba yanapelekea kuingia Motoni au kukaa ndani yake kwa kitambo kirefu. Lakini hata hivyo madhambi hayo hayamtoi mtu nje ya Uislamu, hivyo ukawapata baadhi ya watu wakavunjika moyo. Matokeo yake wakaendelea kuzama ndani ya upotofu. Huu pia ni ufahamu wa kimakosa juu ya maandiko ya makemeo. Kwa ajili hiyo waislamu wamegawanyika makundi matatu juu ya maandiko haya:

1 – Wako ambao wameegemea zaidi upande wa matarajio na kuona kuwa madhambi hayadhuru Uislamu chochote. Hawa ni Murji-ah. Wameegemea upande wa matarajio zaidi kuliko khofu. Wanaona kuwa muumini anaweza kufanya atakacho kwa sababu madhambi hayadhuru imani.

2 – Wako ambao wameegemea zaidi maandiko ya matishio na makemeo. Wanaona kuwa mtenda dhambi kubwa atadumishwa Motoni milele. Kitendo cha watenda madhambi makubwa hawa cha wao kuswali, kutoa zakaah na kuhiji hakijalishi kitu. Hawa ni Mu´tazilah na Khawaarij. Wanasema kuwa mtu akifanya dhambi kubwa kama kwa mfano kuiua nafsi yake, kumuua mwengine, uzinzi au wizi, basi ni mwenye kudumishwa Motoni milele. Makundi yote mawili yamekoseaa.

3 – Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio wako kati na kati ya makundi haya. Wanaona kuyatendea kazi maandiko yote ya Qur-aan na Sunnah, kwa sababu Shari´ah ni moja na ni yenye katika chimbuko moja, kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall); ima kutoka katika Kitabu cha Allaah au kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maandiko hayo yanakamilishana baadhi kwa mengine, baadhi yanafunga mengine na baadhi yanafanya mengine kuwa maalum. Ikiwa kuna maandiko ambayo ni yamekuja kwa njia ya jumla na mengine yamekuja kwa njia maalum, basi inatakiwa kuyafasiri yale ambayo ni ya jumla kwa yale ambayo ni maalum. Ikiwa kuna maandiko ambayo yametajwa kwa njia ya kuachia na mengine yametajwa kwa njia ya kufungamana, basi inatakiwa kufasiri yale maandiko yaliyoachiwa kwa yale yaliyofungamanishwa. Shari´ah na Mweka Shari´ah ni mmoja. Mambo yakishakuwa hivo basi hatuwezi kuchukua sehemu na tukaacha sehemu nyingine. Kwa njia hiyo mtu anakuwa ni mwenye kuepuka matatizo mengine.

Katika Qur-aan Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

“Na yeyote atakayemuua muumini makusudi, basi malipo yake ni Moto ni mwenye kudumishwa humo na Allaah atamghadhibikia na atamlaani na atamuandalia adhabu kuu.”[2]

Hapa kumetajwa adhabu tano: ataadhibiwa ndani ya Moto, atawekwa humo kwa kitambo kirefu, Allaah amemughadhibikia, Allaah amemlaani na amemwandalia adhabu iumizayo. Pindi unaposoma Aayah hii unaona kuwa yule ambaye atamuua muumini kwa makusudi basi atawekwa Motoni kwa sababu Allaah anasema:

وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ

Imâm Muhammad bin Sâlih bin ´Uthaymîn (d. 1421)

“… na Allaah atamghadhibikia… ”

Yule ambaye Allaah amemlaani basi amemweka mbali na rehema Zake, kitu ambacho kinapelekea kuwa haiyumkiniki kabisa akatokwa nje ya Moto na badala yake akaingizwa Peponi. Kadhalika juu ya ile Hadiyth ambayo ameashiria muulizaji kwa yule mwenye kuiua nafsi yake. Ina maana kwamba hatotoka Motoni kabisa. Kwa sababu haya ni maelezo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maelezo yake ni ya kweli ambayo ni lazima yatokee kwa hali yoyote ile. Kwa hivyo tunasema kuwa kujiua ni sababu inayopelekea mtu kudumishwa Motoni milele, kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo Qur-aan na Sunnah vimejulisha kuwa yapo mambo yanayozuia kudumishwa Motoni milele. Mtu ambaye ana imani ndogo kabisa ijapo ni sawa na sisimizi hatodumishwa Motoni milele. Kwa hiyo tunalifasiri andiko la kwanza kwa andiko la pili. Hiyo ina maana kwamba maandiko kuhusu mtu kujiua mwenyewe yametajwa kwa njia ya jumla kwa lengo la kumtishia kitendo hicho, lakini hakuna wataokadumishwa Motoni milele isipokuwa tu makafiri. Hili ni mosi.

Pili ni kwamba baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa maandiko kama hayo yanatakiwa kufahamika kwa udhahiri wake kama yalivyo. Hiyo ina maana kwamba yule mwenye kujiua anaweza kutokuwa na imani pindi anapofanya kitendo kama hicho. Akiwa sio muumini, basi ni kweli kwamba atadumishwa Motoni milele. Kwa sababu anayejiua ilihali ni mzima wa akili, basi mara nyingi ni kwamba amefanya hivo kutokana na sababu; anachotaka ni kuipumzisha nafsi yake kutokamana na majanga yaliyomkumba. Yule anayeoona kuwa kujiua anakuwa amepumzika kutokamana na majanga yanayomkabili basi amepinga kufufuliwa na adhabu za Aakhirah. Akiwa ni mwenye kuyapinga yote hayo basi anakuwa ni kafiri anayestahiki kudumishwa Motoni milele. Ni kitu kisichoingia akilini kwa anayeiua nafsi yake ili aweze kupumzika ile hali nzito aliyomo isipokuwa ni kwa sababu anaona kuwa anaenda katika hali yenye raha zaidi kwake. Kwa msemo mwingine ni kuwa anatishia shaka, au hata kupinga jambo la  kufufuliwa na adhabu za Aakhirah. Kwa hivyo anakuwa kafiri, hivi ndivo wanavofikiria baadhi ya wanazuoni.

Tatu ni kwamba baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa sentesi “ni mwenye kudumishwa Motoni milele” ni makosa kutoka kwa mpokezi[3].

Kwa hali yoyote ni kwamba, tunapasa kutambua kuwa maandiko ya Qur-aan baadhi yanayafunga na kuyafanya maalum mengine, na kwamba hakuna mgongano wowote juu ya maandiko ya Qur-aan na Sunnah.

Kuhusu masuala ya kumtakia rehema, inafaa kumtakia rehema. Kwa sababu sio kafiri, ijapo anaweza kuwekwa Motoni kwa kipindi kirefu mpaka pale atakapotaka Allaah.

[1] al-Bukhaariy (5778) na Muslim (109).

[2] 04:93

[3] Haafidhw Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) amesema:

”Ahl-us-Sunnah wana majibu mengi juu ya hilo. Moja wapo nyongeza hiyo ni ya makosa. at-Tirmidhiy amesema: ” Ameipokea Muhammad bin ´Ajlaan, kutoka kwa Sa´iyd al-Maqbariy, kutoka kwa Abu Hurayrah pasi na ”kudumishwa milele”. Hivo ndivo ilivyopokelewa pia na Abuz-Zinaad, kutoka kwa al-A´raj, kutoka kwa Abu Hurayrah. Hiyo ndio sahihi zaidi kwa sababu imesihi kwamba wapwekeshaji wataadhibiwa kisha baadaye watatowa ndani. Kwa hivyo hawatodumishwa Motoni milele.” (Fath-ul-Baariy (3/327))

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/151-155)
  • Imechapishwa: 23/08/2021