Swali: Mimi ni msichana ambaye tangu hapo kitambo nimekadiriwa kijana fulani na siku hiyo imekutana na wakati nilipokuwa na ada yangu ya mwezi. Lakini sikukubali isipokuwa baada ya kumuuliza mmiliki juu ya kujuzu kwa ndoa katika hali kama hii ambapo mmiliki anakijibu kwamba inajuzu. Lakini hata hivyo sikuridhika na jibu hilo. Naomba unipe faida kama ndoa hii inasihi.

Jibu: Kufunga ndoa na mwanamke katika hali ya hedhi yake ni ndoa inayojuzu na ni sahihi. Ndoa hiyo haina neno. Hilo ni kwa sababu msingi katika ndoa ni uhalali na kusihi muda wa kuwa hakujakuja dalili inayoonyesha juu ya uharamu na kuharibika kwake. Hakukutajwa dalili inayoonyesha kuwa ndoa kipindi cha hedhi ni haramu. Mambo yakishakuwa hivo basi ndoa iliyotajwa inakuwa ni sahihi na wala haina ubaya wowote.

Hapa tunatakiwa kujua tofauti kati ya kufunga ndoa na kutoa talaka. Talaka haifai katika hali ya hedhi; bali ni haramu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alighadhibika wakati alipofikiwa na khabari kwamba ´Abdullaah bin ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amemtaliki mke wake ilihali yuko na hedhi. Matokeo yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha amrejee na amwache mpaka kwanza asafike, kisha apate hedhi, kisha asafike tena, halafu baada ya hapo akitaka abaki naye na akitaka amtaliki. Hayo ni kutokana na maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ رَبَّكُمْ ۖ لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِن بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ۚ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ

“Ee Nabii!  Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa eda [twahaarah] zao na hesabuni eda; na mcheni Mola wenu. Msiwatowe katika manyumba yao na wala wao wasitoke isipokuwa wakileta uchafu wa wazi – na hiyo ndio mipaka ya Allaah; na yeyote atakayevuka mipaka ya Allaah, basi hakika ameidhulumu nafsi yake.”[1]

Kwa hivyo si halali kwa mwanaume kumtaliki mke wake akiwa yuko na hedhi wala kumtaliki katika twahara aliyomwingilia isipokuwa ikibaini kuwa yuko na ujauzito. Kukishabaini ujauzito wake basi inafaa kwake kumtaliki wakati atapotaka na talaka inakuwa ni yenye kupita.

Miongoni mwa mambo ya ajabu ni jambo lililoenea kwa watu wasiokuwa na elimu kwamba talaka haipiti kumtaliki mwanamke mjamzito, jambo ambalo si sahihi. Talaka ya mjamzito ni yenye kupita. Kutokana na hili inafaa kwa mwanaume kumtaliki mwanamke mjamzito ingawa punde tu amemwingilia. Hilo ni tofauti na ambaye si mjamzito akimwingilia basi ni lazima kwake kusubiri mpaka kwanza apate hedhi, kisha asafike au kubaini ujauzito wake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema katika Suurah “at-Twalaaq”:

وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ

“Wale wenye mimba muda wao [wa eda] watakapozaa mimba zao.”[2]

Hii ni dalili ya wazi inayoonyesha kuwa talaka ya mjamzito inapita. Katika baadhi ya matamshi ya Ibn ´Umar imekuja:

“Mwamrishe amrejee; kisha amtaliki akiwa ameshatwahirika au mjamzito.”

Ikishabainika kwamba kufunga ndoa na mwanamke huyu ilihali yuko na hedhi ni ndoa inayojuzu na sahihi, basi mimi naona kuwa asicheze naye mpaka kwanza atwahirike. Hilo ni kwa sababu akicheza naye kabla ya kutwahirika, basi kuna khatari akatumbukia katika makatazo ambayo ni kumjamii mwanamke mwenye hedhi. Huenda asiweze kuimiliki nafsi yake na khaswakhaswa akiwa bado ni kijana. Hivyo asubiri mpaka kwanza atwahirike na amwingilie mke wake akiwa katika hali ambayo anaweza kustarehe naye kwenye tupu ya mbele.

[1] 65:01

[2] 65:04

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (149) http://binothaimeen.net/content/8578
  • Imechapishwa: 05/10/2019