Kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah


Swali: Kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah inajuzu? Kwa kuwa huku kwetu watu wanamchinjia mtu ambaye anaitwa “Mujalliy”. Na tunapowauliza ni nani Mujalliy? Wanasema kuwa ni Nabii katika Manabii wa Allaah. Tunaomba utupe faida.

Jibu: Kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah ni munkari mkubwa na ni Shirki kubwa, sawa ikiwa kachinjiwa Nabii, walii, nyota, jini, sanamu au visivyokuwa hivyo. Kwa kuwa Allaah (Subhaanah) Anasema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

“Sema: “Hakika Swalaah yangu, na Nusukiy (kuchinja kafaara na ‘ibaadah zangu) na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah (Pekee) Mola wa walimwengu. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (waliojisilimisha kwa Allaah).” (06:162-163)

Akaelezea (Subhaanah) kuwa kuchinjiwa ni kwa ajili Yake kama Swalah ilivyo Yake. Atakayechinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, ni kama aliyeswali kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Atakuwa kamshirikisha Allaah (´Azza wa Jalla). Hali kadhalika Anasema (Subhaanah):

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

“Hakika Sisi Tumekupa al-Kawthar (mto katika Jannah). Basi swali kwa ajili ya Mola wako na chinja (kwa ajili Yake).” (108:01-02)

Swalah na kuchinja ni ´Ibaadah mbili muhimu sana. Atakayewachinjia walio ndani ya makaburi, Manabii, nyota, sanamu, jini au Malaika, basi atakuwa amemshirikisha Allaah. Ni kama mfano wa kuswali kwa ajili yao, au kuwataka msaada (kwa wasiyoyaweza) au kuwawekea nadhiri, yote haya ni kumshirikisha Yeye (Subhaanah). Na Allaah (Subhaanah) Anasema:

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba Misikiti ni (kwa ajili) ya Allaah, basi msiombe (msimuabudu) yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

Na Anasema (Subhaanah):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na watu wa isipokuwa waniabudu.” (51:56)

Na Anasema (Subhaanah):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

“Na Mola wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu (yeyote) isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia wema wazazi wawili.” (17:23)

´Ibaadah ni haki ya Allaah Pekee; na kuchinja ni miongoni mwa ´Ibaadah, kutaka msaada ni katika ´Ibaadah na Swalah ni katika ´Ibaadah. Na imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema: “Allaah Amlaani mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah.” (Swahiyh Muslim, Hadiyth kutoka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhu)) Ni juu yenu kuwakataza watu hawa na kuwafunza ya kwamba hii ni Shirki kubwa na kwamba lililo la wajibu juu yao ni kuacha hilo. Hawafai kwao kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, kama ambavyo hawafai kuswali kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Na hili, ni kwa ajili ya kusaidia katika wema na uchaji Allaah, kukataza maovu, na kulingania katika Dini ya Allaah na kumpwekesha Allaah kwa kumtakasia ´Ibaadah Yake. Kwa minajili ya Tawhiyd. Ni wajibu ´Ibaadah iwe kwa Allaah Mmoja (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni wajibu kwa wanachuoni, wanafunzi na Waislamu kusaidiana juu ya wema na uchaji Allaah na wakataze Shirki kwa yule mwenye kuifanya, mpaka iweze kudhihiri Tawhiyd na kushikwe vikwazo kwa sababu zinazopelekea katika Shirki.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb
  • Imechapishwa: 26/03/2018