Kubeba msahafu ndani ya swalah ya Tarawiyh

Swali 282: Ni ipi hukumu ya waswaliji kubeba msahafu katika swalah ya Tarawiyh Ramadhaan kwa haja ya kumfuata imamu?

Jibu: Kubeba msahafu kwa lengo hili ni kwenda kinyume na Sunnah kwa njia zifuatazo:

1- Mtu anapitwa na kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto wakati amesimama.

2- Inampelekea kutikisika sana wakati wa kufungua msahafu, kuufunga, kuuweka kwenye kwapa, mfukoni na kadhalika, mambo yasiyokuwa na haja.

3- Kunamshughulisha mswaliji kwa matikiso haya.

4- Kunamfanya mswaliji kupitwa na jambo la kutotazama pale sehemu anaposujudia. Wanachuoni wengi wanaona kwamba kutazama ile sehemu ya kusujudia ndio Sunnah na bora zaidi.

5- Mwenye kufanya hivo huenda akasahau kuwa yumo ndani ya swalah ikiwa hakuudhurisha moyo wake kwamba yumo ndani ya swalah. Hivo ni tofauti pale atapokuwa ni mwenye kunyenyekea na hali ya kuwa ameweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto na ameelekeza kichwa chake chini. Katika hali hii anakuwa karibu zaidi kujihudhurisha kwamba yuko anaswali na kwamba yuko nyuma ya imamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Arkaan-il-Islaam, uk. 356
  • Imechapishwa: 17/05/2019