Swali: Ni ipi hukumu ya kuapa kwa Ka´bah na mfano wake? Ni zipi formula za viapo vinavyojuzu?

Jibu: Haijuzu kuapa kwa Ka´bah wala kwa viumbe vyengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayetaka kuapa basi na aape kwa Allaah au anyamaze.”[1]

Kumeafikiana juu ya usahihi wake.

“Mwenye kuapa kwa kitu badala ya Allaah ameshirikisha.”[2]

Ameipokea Imaam Ahmad kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

“Mwenye kuapa kwa asiyekuwa Allaah basi amekufuru au ameshirikisha.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Hadiyth zilizo na maana kama hii ni nyingi ambazo zinafahamisha uharamu wa kuapa kwa Ka´bah, amana, Mitume na viumbe vyenginevyo.

Kiapo kilichowekwa katika Shari´ah ni kuapa kwa Allaah peke yake. Kama mfano kusema:

والله

Wallaahi,

بالله

Billaahi,

au

تالله

Tallaahi

nitafanya jambo fulani au kwamba sintofanya jambo fulani. Vivyo hivyo ikiwa mtu ataapa kwa jina tukufu miongoni mwa majina ya Allaah au sifa Zake. Kama mfano wa Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu, mfalme wa wafalme, ninaapa kwa uhai wa Allaah, ninaapa kwa ujuzi wa Allaah na mfano wa hivo.

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mara nyingi akiapa kwa kusema:

“Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake.”

[1] al-Bukhaariy (2679), Muslim (1646), at-Tirmidhiy (1534) na wengineo.

[2] Ahmad (01/47).

[3] at-Tirmidhiy (1535), Abu Daawuud (3251) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/146)
  • Imechapishwa: 02/07/2017