Swali: Wakati mmoja katika Maswahabah alipofariki walihudhuria maziko yake Malaika 70.000, na pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomzika alisema:

“Alibanwa, kisha akaachiwa.”[1]

Je, haya yanaamfika kila mmoja?

Jibu: Swahabah huyo ni Sa´d bin Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh), kiongozi wa Aws. Alikuwa mwenye kushirikiana na Banuu Quraydhwah ambao walipomsaliti Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada ya udanganyifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawapiga vita na kuwazingira kwa zaidi ya nyusiku ishirini. Walipochoka kuzingirwa wakaomba washushwe juu ya hukumu ya Sa´d bin Mu´aadh, maombi ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyakubali. Sa´d bin Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa amejeruhiwa yuko ndani ya hema msikitini. Alikuwa ameumizwa katika vita vya Mahandaki ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjengea hema ndani ya msikiti. Wakati (Radhiya Allaahu ´anh) aliposikia kuwa Banuu Quraydhwah wamevunja mkataba wao akasema:

“Ee Allaah! Naomba usinifishe mpaka Unifurahishe kupitia wao.”

Bi maana alikuwa anataka waadhibiwa kwa kule kuvunja kwao mkataba. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtumia mjumbe kumweleza kuwa washirika wake wanataka kuhukumiwa naye. Akaenda Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh), kutokea msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kwa Banuu Quraydhwah hali ya kuwa amepanda juu ya punda. Alipofika akawaambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Simameni kwenda kwa kiongozi wenu.”

Wakamsimamia na kumshusha. Wale viongozi wa kiyahudi wakamkusanyikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili Sa´d bin Mu´aadh ahukumu kati yao. Mayahudi walikuwa wakitaraji atawahukumu kama ambavo ´Abdullaah bin Ubayy alivowahukumu Banuun-Nadhwiyr. Lakini kulikuwa kuna tofauti kati ya  ´Abdullaah bin Ubayy, ambaye alikuwa kiongozi wa wanafiki, na Sa´d bin Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh). Pindi Sa´d alipohukumu kuwa wanamme wote wapiganaji wanyongwe na wanawake na watoto wao wafanywe mateka, ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Amehukumu kwa hukumu ileile aliyohukumu Allaah kutoka juu ya mbingu ya saba.”[2]

Ndipo ikatekelezwa hukumu yake. Baada ya hapo Sa´d bin Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) akavuja damu na akafariki. Alikufa baada ya Allaah kuipokea du´aa yake na akamfurahisha kupitia wao. Imesihi kwamba ´Arshi ya Mola (´Azza wa Jall) ilitetemeka wakati wa kufa kwake[3]. Hasan bin Thaabit (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

Katu hatujapatapo kusikia ´Arshi ya Allaah kutetemeka kwa ajili ya kifo

isipokuwa Sa´d, Abu ´Amr

Kuhusu kumbana, imepokelewa kwamba kaburi lilimbana, lakini kama sikusahau Hadiyth hiyo ni dhaifu. Kwa sababu Hadiyth ambazo ni Swahiyh zinajulisha kwamba mtu anapohojiwa na Malaika wawili na akajibu yaliyo ya sawa, basi anafanyiwa nafasi kaburi lake. Lakini kama Hadiyth ni Swahiyh, basi inakusudia kwamba inambana pale mwanzoni tu anapoingia; kisha baada ya hapo anafanyiwa nafasi kubwa. Imesemekana pia kwamba kaburi linambana muumini kama ambavo mama mwenye huruma anavomkumbatia mwanae. Kwa msemo mwingine ni kuwa sio kubana kunakoumiza au kusumbua. Tunamuomba Allaah atujaalie sisi na nyinyi kuwa miongoni mwa waja wake wenye furaha.

[1] an-Nasaa’iy (2054). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy (2054).

[2] al-Bukhaariy (3043), Muslim (1768) na Kitaab-ut-Tawhiyd, uk. 769-770, ya Ibn Mandah.

[3] al-Bukhaariy (3803) na Muslim (2466).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/468-470)
  • Imechapishwa: 15/06/2021