Kila mmoja ana jukumu la kuisogeza mbele Da´wah Salafiyyah


Swali: Muislamu na kijana wanatakiwa kuchukua msimamo gani juu ya makundi haya ambayo yanautenganisha Ummah ikiwa ni pamoja vilevile na kundi la al-Ikhwaan al-Muslimuun?

Jibu: Hata kama makundi yatazidi kuwa mengi na kukithiri basi itambulike kuwa hakuna kundi lililo juu ya haki isipokuwa moja tu. Nalo ni lile linalofuata yale waliyokuwemo as-Salaf as-Swaalih ambao ni Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Halitoacha kuwepo kundi kutoka katika Ummah wangu juu ya haki hali ya kuwa ni washindi. Hawadhuriki na wale wenye kuwakosesha nusura na wale wenye kwenda kinyume nao mapaka ifike amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Himdi zote ni za Allaah kuona Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hakutuacha patupu. Bali ametuwekea wazi haki. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro vyenginevyo vitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni  kwayo mpate kumcha.” (06:153)

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ametusimamishia hoja, akatubainishia njia na akatuwekea wazi njia. Haitoshi kwa mtu mwenyewe akaijua na kuitambua haki. Bali ni lazima awafunze na kuieneza kwa wengine. Hii ndio faida ya msomi ajue, afunze na awafikishie watu haki hii kwa kiasi cha uwezo wake. Basi angalau awafunze watu Qur-aan na kuwahifadhisha nayo na vilevile Hadiyth na akaacha maelezo na ufafanuzi wake kwa wanachuoni. Awahifadhishe maandiko na wao wataenda kwa wanachuoni ili wawafafanulie. Kila moja ana jukumu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqiyqatu Da´wat-ish-Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab http://alfawzan.af.org.sa/ar/node/17206
  • Imechapishwa: 30/12/2017