Inafaa kumuombea vibaya mtu aliyekudhulumu?

Swali: Lililo bora kwa mwenye kudhulumiwa aombe dhidi ya yule aliyemdhulumu au afanye sababu zitazopelekea kurudishiwa haki yake khaswa kwa kuzingatia ya kwamba imekuja katika Hadiyth:

“Du´aa ya mwenye kudhulumiwa hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi chochote.”

Hapa kuna ishara kwamba mtu anatakiwa kumkimbilia kumuomba Allaah dhidi ya yule aliyemdhulumu?

Jibu: Mdhulumiwaji ana haki ya kuomba dhidi ya aliyemdhulumu kwa kiasi cha dhuluma aliyomfanyia. Dalili ya hilo ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Iogope du´aa ya mwenye kudhulimiwa. Kwani hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi chochote.”

Wakati fulani yule mwenye kudhulumu anashindwa kumrudishia haki haki yake aliyemdhulumu na kumuwekea mambo uwazi. Inawezekana ni kwa sababu aliyemdhulumu ni ndugu yake, rafiki au mpinzani wake ambaye hawezi kuongea naye juu ya hili. Katika hali hii hana jambo awezalo kufanya isipokuwa kumuombea du´aa.

Lakini ifahamike pia kwamba wakati mwingine mtu anamtuhumu mwenzake kwamba amemfanyia vibaya. Je, mtu huyu ana haki ya kumuombea vibaya kwa Allaah huyu anayemtuhumu au afungamanishe du´aa kwa kusema:

“Ee Allaah! Ikiwa fulani amenidhulumu au amenifanyia vibaya kwa kitu fulani?”

Bora ni hili la pili. Wakati fulani mtu anatuhumiwa kwamba amemfanyia vibaya mtu mwingine au amemroga, lakini mtu huyo hawezi kuongea. Kwa sababu hana dalili yoyote. Lakini viashirio vyenye nguvu vinafahamisha kwamba mtu huyu amemfanyia vibaya. Katika hali hii Mola wa walimwengu ndiye ambaye anakuwa mjuzi. Aseme:

“Ee Allaah! Ikiwa fulani ndiye ambaye amenifanyia hivi… “

Halafu aombe kwa kile ambacho anaona atakuwa amelipiza. Lakini hata hivyo endapo mtu atasubiri, akavuta subira na akamwachia jambo lake Allaah itakuwa ni vyema zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (45) http://binothaimeen.net/content/1036
  • Imechapishwa: 02/03/2019