Imamu ameenda Rak´ah ya tatu katika Tarawiyh kwa kusahau

Swali: Imamu anayeswali Tarawiyh akaenda katika Rak´ah ya tatu kwa kusahau ambapo maamuma wakamkumbusha lakini hata hivyo hakurudi na badala yake akaendelea kuswali hiyo Rak´ah ya tatu na ya nne. Kisha baada ya hapo akatoa salamu na hakusujudu sijda ya kusahau. Je, inafaa kwake kufanya hivo? Ni ipi hukumu ya swalah yake na swalah ya wale walioko nyuma yake?

Jibu: Imaam Ahmad aliulizwa swali hili na akasema kwamba ni lazima kwa imamu kurudi hata kama ameshaanza kusoma, kwa sababu analazimika kutoa salamu[1].

Wanachuoni wameafikiana kwamba kurudi kwake ndio bora na kamilifu zaidi kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbili mbili.”[2]

Lakini wakatofautiana; je, swalah yake inaharibika iwapo hatorudi? Baadhi wanaona hivo. Katika “al-Muntahaa´” imekuja:

“Kitendo cha kunuia kwake Rak´ah mbili za sunnah kisha akainuka kwenda katika Rak´ah ya tatu ni kama kuswali Fajr kwa Rak´ah tatu, kwa sababu Hadiyth inasema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbili mbili.”

Aidha swalah hiyo imewekwa katika Shari´ah kuswaliwa Rak´ah mbilimbili na imeshabihiana na swalah ya faradhi.”[3]

Katika “al-Iqnaa´” imekuja:

“Yule aliyenuia Rak´ah mbili za sunanh usiku na akainuka kwenda katika Rak´ah ya tatu kwa kusahau bora ni kurudi kuliko kuikamilisha Rak´ah nne. Kuikamilisha kunaibatilisha. Kisha baada ya hapo atatakiwa kusujudu sijda ya kusahau. Kama amenuia Rak´ah mbili za sunnah usiku na akasimama katika Rak´ah ya tatu na asirudi, basi swalah yake inabatilika kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbili mbili.”

Midhali swalah imewekwa katika Shari´ah kuswaliwa Rak´ah mbilimbili imeshabihiana na Fajr.”

Maoni sahihi wanavoona wahakiki ni kwamba ni lazima kwake kurejea kutokana na Hadiyth iliotangulia:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbili mbili.”

[1] al-Furuu´ (1/513) ya Ibn Muflih.

[2] al-Bukhaariy (990) na Muslim (749).

[3] al-Muntahaa (1/210).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdil-´Aziyz al-´Aqiyl
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://ar.islamway.net/fatwa/30859/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D9%85%D9%86-%D9%82%D8%A7%D9%85-%D8%A5%D9%84%D9%89-%D8%B1%D9%83%D8%B9%D8%A9-%D8%AB%D8%A7%D9%84%D8%AB%D8%A9-%D9%81%D9%8A-%D8%A7%D9%84%D8%AA%D8%B1%D8%A7%D9%88%D9%8A%D8%AD
  • Imechapishwa: 17/05/2019