Ibn ´Uthaymiyn mtu kujitolea kiungo kabla na baada ya kufa

Swali: Kuna ndugu yangu mmoja amefariki. Je, ni jambo linalokubalika Kishari´ah kupeana moja katika viungo vyake. Ikiwa ni jambo linalokubalika Kishari´ah, bora ni kupeana kiungo hicho au kutokipeana? Allaah akujaze kheri.

Jibu: Sidhani kwamba kuna mtu anaweza kufanya hivi. Maiti akifariki anatakiwa kuheshimiwa kama ambaye yuko hai. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuvunja kiungo cha maiti ni kama kumvunja akiwa hai.”

Wanachuoni wa Fiqh wa madhehebu ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) wametaja kwamba haijuzu kukata kitu kutoka kwa maiti japokuwa maiti ataacha anausia hivo. Kwa mfano maiti kabla ya kufa ameacha anausia kwamba akifa wamtoe ini, moyo, jicho na vyenginevyo. Katika hali hii haijuzu kutekeleza wasia wake.

Kadhalika haijuzu kwa aliye hai kupeana kitu katika viungo vyake. Haijuzu kumpa hata mama na baba yake. Tukadirie kuwa mama ini lake limepoza na madaktari wakathibitisha kwamba ni lazima kwa mtoto wake kumpa ini lake limoja, si halali kwake kufanya hivo. Kwa sababu mtu akitolewa ini moja anabaki na ini moja. Ini hili limoja likipatwa na ugonjwa huenda ikawa ni sababu ya kufa. Kwa sababu ametolewa moja katika mafigo yake.

Kwa hivyo haifai kwa yeyote kupeana chochote kutoka katika mwili wake. Ni mamoja akiwa bado yuko hai wala baada ya kufa kwake. Isipokuwa tu ikiwa kimoja; nacho ni damu. Inajuzu kwa mtu kujitolea damu yake. Kwa sharti asidhurike kwa kule kuchotwa kwake damu. Jengine afaidike na damu hiyo. Tofauti kati yake na kiungo ni kwamba damu inakuja mahala pake nyingine. Mtu anapochotwa damu kutoka kwenye mishipa yake kunakuja mahala pake damu nyingine. Kwa njia hiyo hawi ni mwenye kudhurika kwa kule kuchotwa damu kutoka kwake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (66) http://binothaimeen.net/content/1481
  • Imechapishwa: 29/01/2020