Ibn ´Uthaymiyn kuhusu kofia za chepeo na tarbushi

Swali: Masiku yaliyoisha imekuwa ni jambo lenye kuenea kati ya watoto wa kiume na vijana kuvaa kofia za aina ya chepeo na tarbushi. Ni ipi hukumu ya kuzivaa?

Jibu: Baadhi ya watu wanadai kwamba wanavaa kofia hizi kwa sababu ya kujikinga na mwanga na ukali wa jua. Lakini madai haya hayana ukweli wowote. Kwa sababu tumewaona wenye kuzivaa usiku. Je, usiku kuna jua? Hakuna jua. Lakini ni mtindo.

Halafu jengine ni kwamba mimi nawanasihi ndugu ambao wanazivaa kwamba kufunika macho kiasi hiki kwa njia ya kwamba mtu hawezi kukutana na miale ya jua ni jambo lina madhara kwake sana. Ni kama mtu ambaye kishazowea starehe na anasa ukimwambia atembee kwa miguu kutoka hapa kwenda mpaka sokoni, basi atachoka sana. Lakini mtu ambaye kishajizoweza kutembea kwa miguu si lolote si chochote. Vivyo hivyo viungo vyote vilivyomo mwilini. Ukiyazoweza macho yako kutotaka kutazama miale ya jua basi utambue kuwa hilo lina madhara kwako. Upande wa matibabu ni jambo lina madhara. Isipokuwa ikiwa kama mtu ana matatizo au maradhi ya macho na anataabika kwa mwanga wa jua, katika hali hii pengine mtu akasema kuwa hakuna neno pamoja na kwamba badala yake anaweza kuvaa miwani ya kimatibabu dhidi ya jua.

Naona kuwa katika kuwapendea kheri ndugu na watoto zangu wasizivae. Kwani wako na mavazi mengine mbadala wanayoweza kuweka kichwani na yakazuia ukali wa jua mbali na kofia aina hizi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (56) http://binothaimeen.net/content/1279
  • Imechapishwa: 08/10/2019