Swali: Ni ipi hukumu ya kufunga masiku kumi ya mwisho ya Dhul-Hijjah, mwezi wa Muharram na mwezi wa Sha´baan wote?

Jibu: Kufunga Muharram ni jambo linakubalika katika Shari´ah. Hali kadhalika Sha´baan. Ama kuhusu masiku kumi ya mwisho ya Dhul-Hijjah hakuna dalili juu ya hilo. Lakini ni sawa endapo mtu atafunga bila ya kuamini kuwa yana umaalum. Kuhusu mwezi wa Allaah Muharram itambulike kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Funga bora baada ya Ramadhaan ni mwezi wa Allaah Muharram.”[1]

Mtu akifunga mwezi mzima ni vizuri. Vilevile akifunga ile tarehe tisa, kumi na tarehe kumi na moja hiyo ni Sunnah.

Vivyo hivyo Sha´baan. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiifunga yote kupitia Hadiyth ya ´Aaishah na Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Kuhusu yale masiku kumi ya Dhul-Hijjah, makusudio ni masiku tisa kwa sababu haifai kufunga ile siku ya idi. Kufyafunga masiku haya ni sawa kutokana na ujumla wa maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakuna masiku yoyote ambayo matendo mema yanapendwa zaidi na Allaah kama masiku haya kumi.” Maswahabah wakasema: ”Hata Jihaad katika njia ya Allaah?” Akasema: ”Hata Jihaad katika njia ya Allaah. Isipokuwa tu mtu ambaye ametoka na nafsi yake, mali yake na asirudi na chochote katika hayo.”[2]

Ama kuhusu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imepokelewa ya kwamba alikuwa akiyafunga na imepokelewa vilevile ya kwamba alikuwa hayafungi. Hakukuthibiti kitu katika yale mapokezi yanayothibitisha kuwa alikuwa akiyafunga wala yale mapokezi yanayokanusha kwamba alikuwa hayafungi.

[1] Muslim (1163).

[2] Ahmad (7039).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.binbaz.org.sa/fatawa/625
  • Imechapishwa: 22/08/2017