Hukumu ya wenye kufanya maulidi na mwenye kuyahudhuria

Swali: Ni ipi hukumu ya mazazi ya Mtume na ni ipi hukumu ya mwenye kuyahudhuria? Je, anaadhibiwa mwenye kuyafanya akifa ilihali yuko katika sura hii?

Jibu: Hakukupokelewa kitu katika Shari´ah kinachofahamisha juu ya kuyasherehekea maulidi. Ni mamoja mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala ya mtu mwengine. Tunachojua kupitia Shari´ah takasifu na wakayathibitisha wanachuoni wahakiki ni kwamba kusherehekea maulidi ni Bid´ah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – ambaye ndiye mtu anayewatakia watu kheri zaidi, mjuzi zaidi wa Shari´ah ya Allaah na mwenye mfikishaji kutoka kwa Allaah – hakusherehekea maulidi yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala Maswahabah zake. Si makhaliyfah wake waongofu wala wengineo. Lau yangelikuwa ni haki, kheri na Sunnah basi wangeliyafanya na (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asingeliyaacha. Bali angeliwafunza nayo Ummah wake. Yeye ni mjuzi zaidi wa kujitambua. Jengine ni kwamba Maswahabah zake na makhaliyfah wake wangeliyafanya. Maswahabah zake na makhaliyfah wake (Radhiya Allaahu ´anhum) wangeliyafanya. Walipoacha kuyafanya ndipo tukajua kwa yakini kwamba hayana chochote kuhusiana na Shari´ah. Vivyo hivyo zile karne bora hawakufanya hivo. Kwa hivyo mambo yakawa wazi kwamba ni Bid´ah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote mwenye kuzua katika amri yetu hii yasiyokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”

“Yeyote mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”

Zipo Hadiyth zengine zinazofahamisha juu ya hayo. Kwa hayo tunapata kujua usherekeaji huu wa maulidi haya yanayofanyika katika Rabiy´ al-Awwal na wakati mwingine, kadhalika usherekeaji huu wa maulidi mengine kama mfano wa maulidi ya al-Badawiy, al-Husayn na wengineo yote ni Bid´ah na zenye kukemewa ambazo ni lazima kwa waislamu kuachana nayo.

Allaah amewapa badala ya sikukuu mbili kuu; ´Iyd-ul-Fitwr na ´Iyd-ul-Adhwhaa´. Zinatosha kwa kutohitajia kuzusha sikukuu na sherehe zilizokemewa na zilizozuliwa.

Kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukuwi kwa kufanya maulidi na kuyasimamisha. Kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunapelekea kumfuata, kushikamana na Shari´ah yake, kuitetea, kulingania kwayo na kunyooka juu yake. Haya ndio mapenzi:

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu.”[1]

Kumpenda Allaah na Mtume Wake sio kwa kufanya maulidi wala kwa kufanya Bid´ah. Lakini kumpenda Allaah na Mtume Wake kunakuwa kwa kumtii Allaah na Mtume Wake, kunyooka juu ya Shari´ah ya Allaah, kupambana katika njia ya Allaah, kulingania katika Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuzitukuza, kuzitetea na kumkemea yule mwenye kwenda kinyume nazo. Hivi ndivo inakuwa kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile inakuwa kwa kumuigiliza maneno na matendo yake na kufuata mwongozo wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kulingania katika hayo. Haya ndio mapenzi ya kweli yanayofahamishwa na kitendo kinachoafikiana na Shari´ah.

Kusema kwamba ataadhibiwa au hatoadhibiwa ni jambo jengine ambalo tunamwachia Allaah (Jalla wa ´Alaa). Bid´ah na maasi ni miongoni mwa sababu za adhabu. Allaah anaweza kumuadhibu kwa maasi yake na vilevile anaweza kumsamehe ima kwa ajili ya ujinga wake, amemfuata kichwa mchunga aliyefanya hivo na akafikiria kuwa amepatia, kwa ajili ya matendo mema aliyoyafanya na ndio ikawa ni sababu ya msamaha wa Allaah au kwa ajili ya uombezi wa waombezi kutoka kwa Mitume, waumini au watoto waliokufa kabla ya kubaleghe. Kwa kifupi ni kwamba maasi na Bid´ah ni miongoni mwa sababu za adhabu. Mwenye nayo yuko chini ya utashi wa Allaah (Jalla wa ´Alaa) muda wa kuwa Bid´ah zake sio zenye kukufurisha. Ama Bid´ah zake ikiwa ni zenye kukufurisha na ni shirki kubwa basi mwenye nazo atadumishwa Motoni milele. Lakini midhali Bid´ah ziko chini ya shirki kubwa na bali ni vitaga vinavyokwenda kinyume na Shari´ah katika swalah zilizozuliwa na sherehe zilizozuliwa ambazo ni chini ya shirki ni mambo yako chini ya matakwa ya Allaah kama mtenda maasi.

[1] 03:31-32

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4675/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D9%85%D9%86-%D9%8A%D8%B5%D9%86%D8%B9-%D9%88%D9%8A%D8%AD%D8%B6%D8%B1-%D8%A7%D9%84%D8%A7%D8%AD%D8%AA%D9%81%D8%A7%D9%84-%D8%A8%D8%A7%D9%84%D9%85%D9%88%D9%84%D8%AF-%D8%A7%D9%84%D9%86%D8%A8%D9%88%D9%8A
  • Imechapishwa: 31/10/2019