Hukumu ya Takbiyr wakati mtu anapoinuka katika sijda ya kisomo


Swali: Imamu akisujudu wakati anaposoma Aayah ya kisomo aseme “Allaahu Akbar” na akamilishe kisomo au aunganishe kisomo moja kwa moja pasi na kusema “Allaahu Akbar”?

Jibu: Kama yuko ndani ya swalah basi anatakiwa kusema “Allaahu Akbar” wakati wa kuinama na wakati wa kunyanyuka. Ni mamoja imamu na maamuma. Hapa ni pale anapokuwa ndani ya swalah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akileta Takbiyr kila anapoinama na anaponyanyuka. Akiwa nje ya swalah basi anatakiwa kuleta Takbiyr anaposujudu sijda ya kisomo. Wakati wa kuinuka basi ainuke bila ya Takbiyr wala salamu. Haya yamesihi kutoka kwa ´Umar katika al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah). Kikosi cha wanazuoni wengi wanaona kuwa sijda ya kisomo ni swalah. Kwa hivyo aseme “Allaahu Akbar” wakati wa kuinama na wakati wa kunyanyuka na alete Tasliym kuliani na kushotoni mwake. Maoni ya sawa ni kwamba sio swalah bali ni kumnyenyekea Allaah. Kwa hivyo hana haja ya kuleta Takbiyr wala salamu wakati wa kuinuka.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (20)
  • Imechapishwa: 21/07/2021