Hukumu ya kuswali na viatu


Swali: Ni ipi hukumu ya mwenye kuingia nyumbani kwake na viatu na anaswali navyo msikitini bila kuvivua?

Jibu: Kuswali na viatu ni katika Sunnah. Hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa akiswali na viatu. Lakini kilichowekwa katika Shari´ah ni mtu asiswali navyo mpaka kwanza atazame. Akiona vina uchafu basi avisugue kwenye udongo kisha ndio aswali navyo. Mtu akichelea madhara kwa sababu ya Sunnah hii – kwa mfano akachelea watu wakaja kuidharau misikiti kwa sababu ya kitendo hicho na wakaingia kwa njia isiyokubalika Kishari´ah ambapo ni kule kutotazama viatu vyao na kuviondosha uchafu – basi inaweza kuwa bora zaidi kuiacha kwa sababu ya khofu hii.

Kuhusu yale waliyozowea baadhi ya watu kwa njia ya kwamba wakaingia na viatu vyao msikitini na wakatembea navyo ndani ya msikiti na wao hawakuviangalia kabla ya kuingia msikitini, ni jambo la khatari na lenye kwenda kinyume na Sunnah. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kwa mwenye kuingia msikitini aanze kutazama viatu vyake kabla ya kuingia. Jengine linaloshangaza kwa hawa ambao wanaingia na viatu vyao ni kwamba wanapoingia ile sehemu wanapotaka kuswalia, utawaona wanavivua. Hivyo wameenda kinyume na Sunnah kwa njia mbili:

1- Wameingia msikitini na viatu vyao bila ya kuvitazama.

2- Hawaswali navyo. Bali wanavivua wakati wanapotaka kuswali.

Lililo la wajibu kwa muislamu afuate – katika kutenda na kuacha kwake – yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Asiingie msikitini na viatu vyake isipokuwa baada ya kuvitazama. Akivitazama na akaona vina uchafu basi avisugue kwenye udongo mpaka uchafu uondoke kisha ndio aingie navyo msikitini. Ikiwa hataki kufanya hivo avivue kabla ya kuingia msikitini.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (14) http://binothaimeen.net/content/6790
  • Imechapishwa: 11/02/2021