Hukumu ya kufikiria mambo ya haramu bila kuyafanya

Swali: Ni ipi hukumu ya kufikiria kufanya mambo ya haramu? Kwa mfano mtu anafikiria kuiba au kuzini ijapokuwa anajijua kwamba hawezi kufanya hivo endapo njia itamuuwepesikia?

Jibu: Yanayotokea ndani ya nafsi ya mtu katika fikira mbaya, kama mfano wa kufikiria uzinzi, kuiba, kunywa kilevi au mfano wa hayo na asifanye kitu katika hayo, hakika anasamehewa na wala hapati dhambi kwa jambo hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah ameusamehe Ummah wangu yale yanayonong´onezwa na nafsi zao muda wa kuwa hawakuyafanya wala kuyatamka.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kutamani kufanya jambo ovu na asilifanye hatoandikiwa nalo.”

Katika tamko lingine imekuja:

“… Nitamwandikia jema moja kwa kuwa ameliacha kwa ajili Yangu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Maana yake ni kwamba yule mwenye kuacha ovu ambalo alitamani kulifanya akaliacha kwa ajili ya Allaah, basi Allaah atamwandikia tendo jema. Akiacha kulifanya kutokana na sababu nyenginezo, basi hatoandikiwa dhambi na wala hatoandikiwa tendo jema. Haya ni kutokana na fadhilah za Allaah (Subhaanah) na rehema Zake juu ya waja Wake. Anastahiki himdi na shukurani. zote njema. Hapana mungu wala mola wa haki asiyekuwa Yeye.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (05/424) https://binbaz.org.sa/fatwas/1440/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D8%A7%D9%84%D8%AA%D9%81%D9%83%D9%8A%D8%B1-%D9%81%D9%8A-%D8%A7%D9%84%D8%AD%D8%B1%D8%A7%D9%85-%D8%AF%D9%88%D9%86-%D8%B9%D9%85%D9%84
  • Imechapishwa: 22/12/2019