Swali: Mume wangu anapuuza swalah ya mkusanyiko msikitini na swalah zake nyumbani zinakuwa nje ya wakati ima kwa sababu amelala au kwa sababu anajishughulisha na kitu kitu kisichokuwa na faida. Mimi simwachi na namkumbusha kila wakati kwa kiasi cha kwamba kunatokea kati yangu mimi na yeye mivutano kwa sababu ya hilo. Aidha anasema kwamba Allaah ndiye atamfanyia hesabu juu ya hilo na si mimi ninayestahiki kumfanyia hesabu. Nyumbani kwetu kuna dishi na mimi si mwenye radhi na wala sikai mbele yayo. Bali mume wangu ndiye hukaa mbele yayo na huniacha na anatumia muda wake mbele ya dishi mpaka usingizi anafikia kulala mbele yayo, haji kitandani na hanipi haki yangu kama mke isipokuwa mara chache baada ya kupita miezi mitatu au zaidi pamoja na kutambua kwamba ana afya nzuri na bado ni kijana.

Jibu: Tunamuombea kwa Allaah uongofu, amkinge na shari na amsaidie juu ya kheri na utiifu. Ni lazima kwa mume kumuombea uongofu kwa Allaah (´Azza wa Jall). Amuombee kwa wingi. Hapati dhambi zake midhali wakati fulani anamnasihi. Akiongoka, ni vizuri kwa mume mwenyewe na kwa mke huyo, asipoongoka halaumiwi. Isipokuwa ikiwa kama ataacha swalah kabisa, basi hapo haitojuzu kwake kubaki naye dakika hata moja. Kwa sababu akiacha swalah kabisa anakuwa kafiri aliyeritadi. Kafiri aliyeritadi haijuzu kwake kumwingilia kinyumba mwanamke wa Kiislamu japokuwa alimuoa kwa ndoa sahihi. Akiritadi kwa njia ya kwamba akawa haswali kabisa, basi ni wajibu kuwatenganisha kati yao. Mimi hivi sasa simzungumzii mwanaume huyu ambaye kumeulizwa juu yake hivi sasa, kwa sababu hakutaja kwamba haswali. Udhahiri wa hali yake ni kwamba anaswali lakini hata hivyo anapuuzia swalah. Kwa hivyo tunamwambia mke afanye pupa ya kumuombea uongofu kwa Allaah. Akiongoka basi hilo ndilo litakiwalo na asipoongoka basi hapati chochote katika dhambi zake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (51) http://binothaimeen.net/content/1167
  • Imechapishwa: 04/07/2019