Hivi ndivyo unatakiwa kufanya pindi imamu anapoenda katika Rak´ah ya tano

Hadiyth inasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali pamoja na Maswahabah wake Dhuhr Rakaa tano. Mmoja wao akasema: “Mtume wa Allaah! Je, swalah imezidishwa?” Akasema: “Hapana. Kwa nini?” Akasema: “Umeswali tano.” Kwa hivyo akawa amesujudu Sujuud mbili kwa sababu ya kusahau kisha akasema:

“Hakika mimi ni mtu kama nyinyi. Nasahau kama mnavyosahau. Nikisahau basi nikumbusheni.”

Kwa msemo mwingine anawaambia ya kwamba mlikuwa mnatakiwa mnikumbushe kwa Rak´ah hii nyongeza na kusema:

سبحان الله

“Kutakasika ni kwa Allaah kutokamana na mapungufu.”

Ni jambo linalojulikana. Alisahau (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) jambo ambalo lilipelekea hukumu ya Kishari´ah. Watu wengi wanaenda kinyume na hukumu hii. Mara nyingi tunasikia kunaulizwa maswali mengi yanayokumbushia hali hii; kuna imamu alikuwa anaswali swalah ya Rak´ah nne ambapo akawa amesimama katika Rak´ah ya tano kwa kusahau. Waswaliji wakachukua misimamo tofauti. Kuna ambao walimfuata imamu, wengine wakabaki wamekaa katika Tashahhud na wakafanya Tasliym bila ya imamu, wengine wakabaki wamekaa na kumsubiri imamu ili waweze kufanya Tasliym pamoja na imamu. Ilihali Hadiyth inaonyesha kuwa Maswahabah wote walimfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Rak´ah ya tano na wakatoa Tasliym pamoja naye.

Kwa hivyo ni lazima kwa muislamu pindi anapotumbukia katika hali kama hii amfuate imamu pindi anaposimama katika Rak´ah ya tano. Hatakiwi kwenda kinyume naye, kama tulivyotokea kutaja punde wanavyofanya baadhi yao. Na wala mtu hatakiwi kufuata tafsiri za baadhi ya watu, ya kwamba Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walimfuata kwa sababu walikuwa wanadhani kuwa kumeletwa Shari´ah mpya kwa njia ya kwamba swalah ya Rak´ah nne imeongezwa na kufanywa Rak´ah tano. Vinginevyo wasingelimfuata. Hivyo ndivyo wanavyosema baadhi ya watu. Ni wapi mmeyatoa haya?

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Juddah (34)
  • Imechapishwa: 12/02/2017